Skip to main content





UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI



Fasihi andishi ni tawi la fasihi linalotumia sanaa ya maneno kufikisha ujumbe kwa hadhira kwa njia ya maandishi. Zipo aina nyingi za fasihi andishi, miongoni mwa hizo ni pamoja na hadithi fupi, riwaya, tamthiliya na mashairi.







Maana ya Uhakiki




Dhana ya Uhakiki
Fafanua dhana ya uhakiki




Uhakiki ni kitendo cha kutathimini, kueleza, kuainisha na kutoa maoni juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalum. Hii ina maana kwamba uhakiki wa kazi za fasihi hautoki katika ombwe, kuna kanuni na taratibu mbalimbali zinazoongoza kufanya uhakiki, na hii ndio sababu kuna nadharia kadha wa kadha za uhakiki wa kazi za kifaishi. AU kwa lugha rahisi tunaweza kusema, uhakiki ni uchambuzi wa kina wa kazi za fasihi kama vile riwaya, tamthiliya na mashairi kwa lengo la kufafanua vipengele vya fani na maudhui.





Misingi ya Uhakiki
Elezea misingi ya uhakiki




Kwa ujumla mhakiki wa kazi za fasihi anapofanya uhakiki wa kazi za kifasihi, huwa analenga vipengele viwili. Pengine analenga kuhakiki fani ya kazi husika au maudhui ya kazi hiyo na wakati mwingine vyote viwili. Kwa hiyo kupitia vipengele hivi ndipo atachambua vitu vingi kama vile ujumbe, falsafa, matumizi ya lugha, dhamira, mandhari na kadhalika.




Kuhakiki Fani



Katika utunzi wa kazi za kifasihi, Fani hutumika kama nyezo ya kuwasilisha mawazo ya mwandishi kwa njia ya kisanaa zaidi. Fani ni mbinu anayoitumia mwandshi ili kufikisha ujumbe kwa watu aliowakusudia.



Vipengele vya fani ni pamoja na wahusika, mandhari, lugha, muundo na mtindo.




Mtindo



Mtindo ni mbinu ya kipekee kifani na kimaudhui, zinazotofautisha msanii mmoja na mwingine. Kwa mfano, namna msanii anavyotumia lugha, anavyoteua msamiati, namna anavyosimulia hadithi yake (anaweza kutumia nafsi ya kwanza, ya pili au ya tatu). Kwa mfano katika riwaya ya “Barua Ndefu kama hii” iliyoandikwa na Mariama Ba ametumia mtindo wa barua ya kirafiki kuanzia mwanzo hadi mwisho, hii pia inaonesha mtindo wake wa kipekee.




Muundo



Muundo ni mpangilio wa kiufundi anaoutumia mwandishi katika kupangilia kazi yake. mpangilio na mtiririko wa kazi ya fasihi, kwa upande wa visa na mtukio.



Kuna aina mbili za kupangilia matukio

Msago, hii ni namna ya moja kwa moja ya kusimulia matukio, yaani kuanzia tukio la kwanza hadi la mwisho kwa namna yalivyotukia. Huu ni muundo wa moja kwa moja.
Urejeshi, huu ni usimuliaji wa kurukaruka hatua, yaani msimuliaji anaweza kuanzia katikati, akaja mwisho na kumalizia na mwanzo




Wahusika



Wahusika ni watu au viumbe ambavyo mwandishi wa fasihi huwatumia ili kufanikisha ujumbe kwa jamii husika. Katika kazi ya fasihi mwandishi huwagawa wahusika katika makundi mawili yaani wahusika wakuu na wahusika wadogo.



Wahusika wakuu ni wale ambao wanajitokeza kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa kazi ya fasihi. Wahusika wadogo ni wale wote ambao wanajitokeza sehemu mbalimbali katika kazi ya fasihi kwa mfano, mwanzoni mwa kitabu hadi mwishoni mwa kitabu.



Wahusika hawa wawe ni wakuu au wadogo wanaweza kugawanyika katika makundi yafuatayo:

Mhusika mviringo ni mhusika ambaye anabadilika kitabia na kimawazo kulingana na hali halisi ya maisha. Kwa mfano wanaweza kuanza kama watu wema lakini hali ya maisha ikawabadilisha na kuwa watu wabaya au wanaweza kuanza kama watu wabaya na hali ya maisha ikawabadilisha na kuwa watu wema.
Mhusika bapa ni mhusika ambaye habadiliki kulingana na hali halisi ya maisha. Mfano; kama ni mwema basi atakuwa mwema kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho na kama ni mbaya basi atakuwa mbaya kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho.
Mhusika shinda yuko katikikati ya mhusika papa na mviringo. Huongozwa na matendo ya hao wahusika wawili. Hajitokezi na msimamo wake imara.




Mandhari



Mandhari hii ni sehemu ambayo matukio ya hadithi au masimulizi hutokea. Mandhari huweza kuwa halisi kama vile baharini, njiani, msituni, kijijini, mijini au ya kufikirika kama vile kuzimu, mbinguni, peponi n.k.




Lugha



Lugha ndio nyenzo kubwa ya msanii katika kazi za fasihi, miongoni mwa vipengele vya lugha ni tamathali za semi pamoja na semi.




Fani za Lugha

Tanakali za Sauti:Ni mbinu ya kutumia maneno yanayoiga sauti au hali fulani au namna kitendo kilivyofanyika.
Tashbiha: Hii ni mbinu ya lugha inayolinganisha vitu au hali mbili tofauti kwa kutumia maneno ya kulinganisha; ‘kama’, ‘mithili ya’, ‘sawa na’, ‘ja’. mfano, Mwembamba kama sindano.
Tashihisi: Hii ni mbinu ya kupatia kitu kisicho hai sifa za kiumbe mwenye uhai (sifa za kibinadamu). Mfano, "Sungura aliposhindwa, akasema sizitaki hizi mbichi".
Takriri: Ni mbinu ya kurudiarudia neno moja au kifungu cha maneno ili kusisitiza ujumbe fulani. Mfano, alikimbia, alikimbia, alikimbia hadi akashika nafasi ya kwanza.
Ukinzani: Ukinzani ni mbinu ya kusisitiza ujumbe kwa kuambatanisha maneno ya kinyume au yanayokinzana.
Sitiari: Ni mbinu ya kulinganisha vitu viwili moja kwa moja kwa kutumia kiungo ‘ni’ ama ‘kuwa’. Mfano; Maisha ni mlima, juma ni mwamba.
Taswira: Ni matumizi ya lugha/maneno yanayojenga picha ya hali au jambo fulani kwa msomaji.
Taashira: Ni matumizi ya lugha ya ishara kuwakilisha ujumbe fulani. Jina au kitu fulani kinatumika kumaanisha kitu kingine chenye uhusiano na kile kilichotumiwa.
Jazanda: Ni kulinganisha vitu viwili moja kwa moja bila kutumia viunganishi.Mfano Bwana Juma alioa kasuku.
Majazi: Majazi ni pale tabia za wahusika zinapoambatana na majina yao halisi.
Lakabu: Ni mbinu ya mhusika kupewa/kubandikwa jina na wahusika wengine ama yeye mwenyewe kujibandika jina linalooana na tabia/sifa zake.
Chuku: Ni kutumia maneno yaliyotiliwa chumvi ili kusisitiza ujumbe fulani au kusifia kitu, kutilia Chumvi.




Semi



Ni fungu la maneno linapotumika kutoa maana nyingine, badala ya ile ya maneno yaliyotumika. Semi hutumika kuficha ukali wa maneno au kupamba lugha. Kuna aina mbili za semi:

Nahau ni usemi unaotumia maneno ya kawaida kwa lengo la kufikisha maana iliyotofauti na maana ya kawaida ya maneno hayo. Nahau huwa na vitenzi.
Misemo ni semi fupifupi ambazo hutumiwa mara kwa mara kwa lengo la kuleta maana maalumu. Misemo haina vitenzi.

Maswali ya Balagha: Tashititi au maswali ya balagha ni maswali yanayoulizwa na msimulizi au mhusika ambayo hayahitaji jibu.
Uzungumzi Nafsiya: Mhusika hujizungumzia, ama kwa kuongea au kuwaza, bila kukusudia kusikika na yeyote.
Ritifaa: Mbinu ya kuzungumza na mtu aliyekufa (au asiyekuwepo) kana kwamba yuko pamoja nawe.
Kuchanganya Ndimi: Kuweka maneno yasiyo ya Kiswahili katika sentensi ya Kiswahili. Mfano, "alisimama kwanza kwa muda, before he went aliniambia nisimwambie mtu yeyote yule, you know!"
Kuhamisha Ndimi: Ni kuingiza sentensi ya lugha nyingine katika kifungu cha lugha ya Kiswahili. Kinyume na Kuchanganya ndimi (ambapo mwandishi huchanganya maneno katika sentensi moja, katika kuhamisha ndimi, sentensi kamilifu ya lugha nyingine hutumika miongoni mwa sentensi za Kiswahili sanifu. Mfano: Kazi hii ni ngumu sana, sitaweza kuifanya. People are trying to convince me to stay here but I think I can't, I must go!
Methali: Methali ni misemo ya hekima yenye maana iliyofumbwa. Mhusika, mwandishi wa fasihi anaweza kutumia methali kupitisha ujumbe.




Mbinu nyingine za Kisanaa

Kinaya ni mambo katika sanaa kuwa kinyume na matarajio ya hadhira.
Kejeli ni mbinu ya sanaa inayotumia maneno kudharau au kukemea kitendo au mtu fulani.
Taharuki ni mbinu ya kusimulia au kuandika riwaya/hadithi kwa kufanya hadhira na/au wahusika wajawe na hamu ya kutaka kujua kitakachotokea baadaye; hamu ya kutaka kuendelea kusoma/kusikiliza. Baadhi ya hadithi huishia kwa taharuki na kuilazimisha hadhira yake ijikamilishie au ibaki ikijiuliza maswali.
Sadfa ni kugongana kwa vitendo viwili vinavyohusiana kana kwamba vilikuwa vimepangwa, japo havikuwa vimepangiwa.
Kisengere Nyuma, Mwandishi ‘hurudi nyuma’ na kuanza kusimulia kisa kilichokuwa kimetendeka kabla ya alichokuwa akisimulia. Aidha, mwandishi hubadilisha wakati wa masimulizi na kuwa wakati wa kisa hicho. Hutumika sana kuonyesha mhusika anapokumbuka kitu, au kutupatia msingi wa jinsi mambo yalivyoanza.
Kisengere Mbele, Mwandishi anapobadilisha wakati na kusimulia mambo yatakavyokuwa siku za usoni; au kutumia lugha isiyo moja kwa moja kutabiri yatakayojiri. Utabiri.




Kuhakiki Maudhui



Maudhui katika kazi ya fasihi ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Maudhui hujumuisha mawazo pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi akatunga na kusanii kazi fulani ya kifasihi. Vipengele vya maudhui ni pamoja na dhamira, migogoro, falsafa ujumbe na msimamo.

Dhamira; hili ni wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Dhamira ni sehemu tu ya maudhui na aghalabu dhamira kuu ndio hujenga kiini cha kazi ya fasihi. Dhamira zimegawanyika katika makundi mawili, kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo.
Migogoro; hii ni mivutano na misuguano mbalimbali katika kazi za fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati ya wahusika, familia zao, matabaka yao, au hata katika nyadhifa mbalimbali. Vilevile migogoro yaweza kuwa ya kiuchumi, kijamii, mogogoro ya nafsi, na migogoro ya kisiasa ambayo hujitokeza katika mitazamo tofauti kulingana na mtiririko wa visa na matukio yanavyopangwa na mwandishi.
Ujumbe; mwandishi anapoandika kazi yake huwa na ujumbe ambao hutaka uifikie jamii aliyoikusudia. Ujumbe katika kazi fasihi ni mafunzo mbalimbali ambayo hupatikana baada ya kusoma kazi ya fasihi. Katika kazi ya fasihi dhamira kuu hubeba ujumbe wa msingi na dhamira ndogondogo hubeba ujumbe ambao husaidia kuujenga au kuupa uzito zaidi ujumbe wa msingi.
Msimamo; katika kazi ya fasihi, mawazo, mafunzo na falsafa ya msanii hubainisha msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Msimamo ni ile hali ya mwandishi kuamua kufuata na kushikilia jambo fulani. Jambo hili huweza kukataliwa na wengi lakini akalishikilia tu. Msimamo ndio huweza kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi wanaoandika kuhusu mazingira yanayofanana. Kwa mfano, katika tamthilia ya “Pesa zako zinanuka” mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi kwani amejadili matatizo yanayochangia kukwama kwa ujenzi wa jamii mpya.
Falsafa ni mawazo ya busara yenye kutawaliwa na misingi mahususi juu ya asili na maana ya ulimwengu na maisha ya mwanadamu. Ni msimamo wa msanii katika maisha juu ya utatuzi wa matatizo katika jamii. Falsafa ya mwandishi inaweza kujulikana kwa kusoma kazi zake zaidi ya moja.
Mtazamo ni hisia au uelewa wa mwandishi juu ya jambo fulani. Kwa mfano anaweza kutazama jambo fulani kwa mtazamo wa kidini, au anaweza kutazama jambo fulani kwa mtazamo wa kisiasa au kisayansi.
Mafunzo; ni mawazo ya kuelimisha yanayopatikana katika dhamira mbalimbali za kazi ya fasihi.




Kufaulu na Kutofaulu kwa mwandishi



Kufaulu au kutofaulu kwa mwandishi kunategemea jinsi alivyoweka uwiano mzuri kati ya fani na maudhui kwa namna ambavyo inaleta uhalisia. Mfano, endapo msanii atakuwa na mhusika Mkongo lakini akawa anazungumza kiswahili kilichojaa misemo na nahau alafu kimenyooka kama mtu wa pwani itakuwa vigumu kusema amefaulu kwani hakuna uwiano mzuri kati ya mhusika mwenyewe na lugha anayoitumia. Kiswahili cha Kongo ni tofauti kabisa na kiswahili kinachozungumzwa na watu wa pwani (Tanzania).





Uhakiki wa Fani katika Kazi za Fasihi Andishi




Uhakiki wa Fani katika riwaya ya Takadini
Hakiki fani katika riwaya ya Takadini




MWANDISHI: BEN J. HANSON



WACHAPISHAJI: MATHEWS BOOKSTORE AND STATIONARIES



MWAKA: 2004




JINA LA KITABU



Jina la kitabu TAKADINI lina maana ya “Sisi tumefanya nini”. Hili ni jina ambalo Sekai alimpa mwanae mara baada ya kumzaa. Jina hili lilitokana na majonzi aliyokuwa nayo juu ya kutaka kuuawa kwa mwanae na yeye ilihali hawakuwa na hatia, ila tu kwa sababu ya mila za jamii yake zilivyotaka. Jina hili la kitabu ni sadifu kwani linasawiri vyema maudhui yaliyomo katika kitabu hiki. “Sisi tumefanya nini?’ ni swali ambalo linatokana na ukosefu wa haki ya kuishi, kubaguliwa kutopendwa, na hata kutengwa kwa watu wenye matatizo katika jamii. Swali hili linawaelekea wanajamii ambao bado wanashikilia mila potofu zinazowakandamiza na kuwanyanyasa watu wenye matatizo mfano, ulemavu wa ngozi, wagonjwa nk. Jina hili pia ni sadifu kwa maisha ya jamii yetu ya watanzania kwani watu bado wanashikilia mila potofu ambazo si nzuri. Mwandishi ametumia jina hili makusudi ili kutaka kuionesha jamii hali halisi ya vilio vya albino, wasichana wadogo wanaolazimishwa kuolewa nk. Kuwa huu sasa ni muda mwafaka wa jamii kuyaacha na kutupilia mbali mambo hayo.




MUUNDO



Muundo alioutumia mwandishi wa riwaya hii ni muundo wa msago au kwa jina lingine muundo wa moja kwa moja. Ameyapanga matukio katika mtiririko sahili kwani ameanza kutuonesha toka mwanzo mpaka mwisho wa maisha ya kijana Takadini “Msope”.Toka kutungwa kwa mimba yake, kuzaliwa kwake na kuishi kwake, matatizo na changamoto zinazomkumba na jinsi anavyokabiliana nazo na hatma ya maisha yake.



Mgawanyo wa visa na mtukio umepangwa katika sura ambapo visa vimejengwa kwa ufundi na kuvifanya vijengane na kukamilishana kuelekea kilele cha masimulizi. Matukio haya yamewekwa katika sura kumi na tatu.

Sura ya Kwanza: Sura hii inaanza kutuelezea kuhusu mwanamke Sekai anavotunga mimba, pia tunaelezwa kuhusu mtazamo mbaya wa wake wenzie juu ya mimba hiyo baada ya Sekai kukaa kwa muda mrefu bila ya kujaliwa mtoto.
Sura ya Pili: Hapa tunasimuliwa jinsi Sekai anavyofanikiwa kujifungua salama. Lakini kwa bahati mbaya kwa kawaida ya jamii yao anajifungua mtoto Zeruzeru ambaye kwa mila zao mtoto huyo ni laana. Hivyo alipaswa kutupwa mara moja ama kuuawa. Hakuna ambaye alikuwa tayari kumpokea mtoto yule kwani si baba yake wala jamii yake ila mama yake pekee.
Sura ya Tatu: Jamii bado haipo tayari kumpokea mtoto Sope, wanawake wenza wa Sekai wanasubiri kwa hamu kuona tukio la kutupwa kwa Takadini litakavokuwa, kwani ndio jinsi mila na taratibu za mababu zilivyotaka. Kutokana na hali hii ndipo Sekai anapata wazo la kutoroka. Anaamua kuondoka kwenda mbali ili kukinusuru kichanga kisicho na hatia kwani alisubiri kwa hamu na uchu wa muda mrefu kupata mtoto.
Sura ya Nne: Sekai anafanikiwa kutoroka na mwanae Takadini ili kumuepusha na kifo, jamii na Mtemi wanapata habari ya kutoroka kwake. Upelelezi unafanyika lakini juhudi hazikuzaa matunda kumpata Sekai na mwanae mchanga waliotakiwa kuuawa. Sekai anasafiri mbali na kufikia kijiji kingine na kupokelewa na mzee Chivero.
Sura ya Tano: Sekai anapokelewa katika kijiji cha mzee Chivero, jamii na wazee wanashitushwa sana na ujio huo lakini wanalazimika kumpokea tu baada ya malumbano ya muda mrefu. Kwani mila ziliwataka kutowatelekeza wageni katika kijiji chao, na hiyo ndiyo inakuwa mwanzo wa matumaini ya Sekai kuhusu kuishi kwa mwanae ambaye alionekana kuwa ni laana ya mababu na hakupaswa kuishi.
Sura ya sita: Baada ya Sekai kupokelewa katika kijiji cha mtemi Masasa, habari za ujio wake zinaenea kwa wanakijiji wote na wanaonekana kushtushwa sana, si hivo tu bali pia wanajiapiza katu kutomsogelea Sope kwani waliamini amelaaniwa. Lakini kwa juhudi za mzee Chivero baba mpya mlezi wa Takadini Sekai anapata rafiki. Tendai mke wa mtemi Masasa. Anajengewa kibanda cha kuishi yeye na mwanae na maisha yanaanza.
Sura ya saba: Sekai anaanza kujishughulisha na shughuli za kawaida kama mama na mwanamke, analima bustani na kufanya kazi ndogo za nyumbani. Siku moja katika safari ya kurudi nyumbani kwa bahati mbaya wanavamiwa na nyuki na kujeruhiwa vibaya yeye na mwanae, anaamua kumtupia mwanae kichakani ili kumuokoa na yeye kujitumbukiza mtoni. Wote wawili wanafanikiwa kutibiwa na kupona majeraha.
Sura ya nane: Taratibu Takadini anaanza kukua lakini anagundulika kuwa hawezi kutembea vyema kwa mguu mmoja, hii ilitokana na kuvunjika Mguu baada ya kurushwa kichakani na mamaye kama juhudi za kumwokoa. Hali hii inamhuzunisha zaidi Sekai na Chivero kwani walimpenda sana. Hapa ndipo mapenzi ya Chivero yalianza kudhihirika rasmi kwa Takadini kwani alijenga urafiki naye na kumpenda kama mwanae. Alimfundisha utabibu wa dawa za kienyeji na mambo mengine mengi. Pia tunaona watoto jinsi walivyombagua Takadini kutokana na hali yake, kwani waliambiwa na wazazi wao wasicheze naye amelaaniwa hivo hawakuthubutu.
Sura ya tisa: Katika sura hii, Mzee Masasi anafariki dunia na kumuacha mzee Chivero katika majonzi makuu. Hali ya mzee Chivero nayo inaanza kuzorota kwa uzee. Anampa Takadini usia mbalimbali na kumfunza. Pia tunaelezwa juu ya fikra mpya za Takadini za kupiga “mbira” kifaa cha muziki cha kijadi, hii baada ya kuvutiwa na sanaa hiyo aliposhiriki sherehe za mavuno za mwaka. Jamii bado ilimtenga Takadini na kumbagua, walimwona si binadamu bali mzuka tu! Na kwa bahati mbaya mzee Chivero naye aliaga dunia na kuacha simanzi kuu kwa Sekai na Takadini mbao alikuwa ni tegemeo na faraja kwao.
Sura ya kumi: Baada ya kifo cha mzee Chivero, Takadini anapata mwalimu maarufu mpiga mbira mzee Kutukwa, anamfundisha kupiga mbira, Takadini anaonesha juhudi kuu na kufanikiwa. Pia anmsaidia kifaa cha kumsaidia kutembea kutokana na mguu wake mbovu, hii inakuwa ni faraja kubwa kwa Takadini na mamaye.
Sura ya kumi na moja: Hapa tunaelezwa juu ya kijana Nhamo adui mkuu wa Takadini kwani hakumpenda na alimdhihaki na kumdhalilisha mara kwa mara. Kijana huyu anaonekana kuwa ni shujaa katika jamii yake kwa kitendo cha kumuua simba mla mifugo. Hiyo inamletea sifa kubwa na majivuno mengi hivo wasichana wengi kumtamani awaoe, hali ni tofauti kwa Shingai ambaye anaonesha hisia za mapenzi kwa Takadini pamoja na hali yake ya “Usope”. Chemchemi za mapenzi ya Takadini kwa Sekai zinaanza kumea jambo ambalo linamkera sana Nhamo na kuzidisha chuki kwa Takadini kwani pia alitamani kuwa na Shengai binti mrembo. Jamii inafanya kikao kujadili suala la Shengai kumpenda Takadini na wanalipinga vikali suala hilo.
Sura ya kumi na mbili: Nhamo anakata shauri na kwenda kumposa Shengai, wazazi wa pande zote mbili wanaliunga suala hilo mkono asilimia zote. Kwani hilo lingewanusuru aibu ya mwanao kuolewa na Sope, kwani walijua fika Shingai alimpenda Takadini na hakumtaka Nhamo. Nhamo anamuonya vikali Takadini kuwa asiendelee na lolote kwa Shengai. Pia hapa zinafanyika sherehe ya kijadi ya kumkaribisha hayati mzee Chivero tena nyumbani.
Sura ya kumi na Tatu: Wakati wa sherehe ya mavuno, binti Shengai anashindwa kuvumilia na kuamua kumfuata Takadini kibandani kwake. Anaamua kuvunja mila za kwao kwani alimpenda kwa dhati Takadini, pamoja na dharau, kejeli, kubaguliwa, ulemavu wake na kuonekana kuwa ni mtu aliyelaaniwa. Wazazi wake wanamtenga na kutomtambua kama ni mtoto wao tena. Suala hilo linatikisa jamii ya watu wa kijiji kile na hata kutaka kuwafukuza Sekai na mwanae lakini wanaokolewa na maamuzi ya busara ya wazee kwa kuwacha Shengai na mpenziwe Takadini waishi hali wakisubiri matokeo! Kuwa je mtoto atazaliwa sope? Na kuongeza ukoo wa masope na kijiji chao kuwa cha masope? Hapa ndio inapojulikana hatma ya Takadini na mkewe kwani anapata ujauzito na kufanikiwa kujifungua mtoto salama asiye Sope. Ilikuwa furaha kuu kwa mama na mtoto na wote pia. Wanaamua kurudi kijijini kwao walikotoroka ili kwenda kuwadhihirishia kuwa hata sope anaweza kuishi hapaswi kubaguliwa na kutengwa




MTINDO



Mwandishi ametumia mitindo kadha wa kadha ili kuipamba kazi yake na kuifanya ivutie wasomaji; mfano matumizi ya nafsi mbalimbali, matumizi ya nyimbo nk.




Matumizi ya nafsi



Kwa kiasi kikubwa yametawala matumizi ya nafsi ya tatu umoja na wingi katika sura zote.Mfano.uk. 30. “ aliingia ndani na kuanza kazi.”Piauk.3 “ Sekai alikoka moto nje ya kibanda, akaketi na kuzungumza na Pindai”.




Matumizi ya nafsi ya pili au dayalojia



Mfano uk 29 - 30. Mazungumzo kati ya Chivero na Sekai:“je umelala salama?“je umelala salama?Sijambo mwanangu, sijui wewe?Sijambo Sekuru,Na mwanao je?Naye hajambo.”




Matumizi ya nafsi ya kwanza. Mfano uk. 82 na 83



“lakini ghafla nilipata nguvu mpya”;“nilikuwa na nguvu kama kijana….”



Pia mwandishi ametumia nyimbo katika baadhi ya sura ili kuwaburudisha na kuliwaza wasomaji. Mfano uk. 2 wimbo aliouimba mke mwenza wa Sekai Rumbdzai.



“Mashamba yetu yamelimwa mbegu nazo zimepandwa zimechipua na kumea, sisi watatu tumepanda mavuno yetu; mheshimiwa wetu amemiliki mavuno kwa mikono yake halisi kutoka mashamba yetu yote lakini ni kipi alichoambulia kutoka ardhi ile isiyomea kitu?”pia ametumia wimbo uk. 34, 57, 85.



Matumizi ya hadithi ndani ya hadithi pia ni mtindo mwingine wa usimulizi alioutumia mwandishi.Mfano uk 82 Kutukwa alisimulia vijana hadithi enzi ya ujana wake na jinsi alivopambana na maadui vitani.




Matumizi ya Lugha



Lugha aliyotumia mwandishi ni lugha fasaha na rahisi inayoeleweka kwa wasomaji wake. Ametumia pia lugha nyinginezo kama vile lugha za kikabila.Maneno kama vile“Amai”,lenye maana ya mama, “Sope” lenye maana yazeruzeru, “shumba”- simba, “mbira” – chombo cha asili cha muziki, “gudza” – blanketi lililotengenezwa kwa nyuzi za magome ya miti.nk.Hivyo mwandishi ametumia lugha hii ili kuwaleta wasomaji kwenye mazingira halisi ya kiutamaduni ya jamii ile.




Matumizi ya tamathali za Semi

Tashibiha: Mfano uk. 6 “ muda huenda polepole mithili ya mwendo wa kakakuona Uk.15 “ habari njema huchechemea kwa mguu mmoja lakina mbaya hukimbia kama Sungura”Uk.16 “….. alibaki kama kinyago cha mpingo”.Uk.28 “ sio kufurika kama Chura”Uk.33 “aligeuza shingo yake sawa na Mbuni”Uk.42 “ nywele kama vinyweleo vya mahindi yaliyokaribia kukomaa”Uk.82 “muziki ulikuwa kama chemchemi ya maji mwilini mwake”
Tashihisi: Mfano uk. 5 “ndege mbalimbali wakiimba kuikaribisha siku mpya” Uk. 7 “vivuli vya jioni viliongezeka urefu” Uk. 18 “maneno yananila mifupa yangu”Uk 25 “kifo kilinukia”
Tafsida: Mfano, uk. 83 “sehemu zake za siri”
Sitiari: Mfano, uk. 88 “Tapfumaneyi aligeuka mbogo” Uk.97“mwana Mbwa hakuiba mfupa”, Tawanda mfupa ulikwenda wenyewe kuchezanaye.” Hapa mfupa umefananishwa na Shingai na Takadini ndio mwana mbwa




Matumizi ya Semi

Methali: Uk. 45 “ kipofu huwa hachagui shimo la kutegea wanyama”uk.33 “ moyo mwema utakufanya uuwawe”
Misemo: Mfano.Uk. 12 “kufikiri katika siri ni sawa na safari ya mbwa”Uk. 100 “kanga hawezi kutua juu ya bua la mtama”Uk.101 “kibuyu kikubwa hakikosi mbegu ndani”Uk. 125 “fuvu la nyani limekuwa kijiko kwa mlo wa mahindi”
Nahau: uk. 27 “ penzi langu kwake halikufua dafu”Uk. 88 “kutiana moyo wa ari”




Matumizi ya mbinu nyinginezo za kisanaa

Nidaa: Mfano,Uk.4 “Ha!” , “Ha! Atimuliwe tena? Mchawi?” Uk.16 “Mai, Wee!” Uk.39. “Ha! Iwe! Ha!”
Mdokezo: MfanoUk.3 “ndiyo Pindai, ninaogopa……….” Uk.42 “mtu mzima kama watu wenine ameamua………”
Takriri: Mfano,uk 57 “ mwanangu, mwanangu, mwanangu, wamekufanya nini?”




Wahusika



Sekai

Ni mke wa Makwati wa kwanza.
Ni mwanamke jasiri.
Anapinga mila potofu na mbaya za jamii yake.
Ni mvumilivu.
Ni mchapakazi mzuri.
Anajifungua mtoto zeruzeru ambaye ni laana kwa jamii yake.
Ni mtiifu na mwenye adabu.
Ana huruma na mnyenyekevu.
Ana mapenzi ya dhati.
Anafaaa kuigwa na jamii.



Takadini

Ni mtoto anayezaliwa na ulemavu wa ngozi( albino)
Anasadikika kuwa ni laana kwa jamii yake hivyo kupaswa kuuawa au kutupwa mbali.
Anaokolewa na mama yake kwa kutoroshewa katika kijiji kingine.
Anapokua anakua kijana jasiri.
Hapendwi na jamii.
Anabaguliwa na jamii, hana rafiki.
Ni mvumilivu na msikivu mwenye heshima.
Alimpenda Chivero sana.
Alikuwa mpiga mbira (chombo cha muziki cha kijadi) maarufu.
Alimuoa Shingai na kupata mtoto asiye Sope.



Makwati

Mume wa Sekai.
Ameoa ndoa ya mitara ana wake wanne.
Anashikilia mila na desturi potofu.
Hana mapenzi ya dhati kwa mwanae.
Hafai kuigwa na jamii.



Dadirai na Rumbidzai

Wake wengine wa mzee Makwati.
Wana wivu.
Hawampendi Sekai.
Wana roho mbaya kwani wanamwombea Sekai mabaya.
Ni katili kwani wanashinikiza Sekai na mwanae wauawe bila huruma.
Wasengenyaji.
Hawafai kuigwa na jamiii.



Pindai

Mke wa pili wa Makwati.
Ana upendo wa dhati kwa Sekai.
Ni mkweli.
Hana wivu.
Ni mshauri mzuri.
Anafaa kuigwa na jamii.



Chivero

Ni mzee wa kijiji cha mzee Masasa.
Anawapokea Sekai na mwanae baada ya kutoroka kwao kwa ukarimu mkubwa.
Ni mwenye roho nzuri.
Ana huruma sana.
Ni mganga wa tiba za asili.
Ana mapenzi ya dhati kwa Takadini na Sekai.
Anamrithisha Takadini uganga.
Ana busara na hekima.
Ni mshauri mkuu wa Mtemi Masasa.
Anafaa kuigwa na jamii.



Mtemi Masasa

Ana busara na hekima.
Ana huruma.
Anafuata mila na desturi ya jamii yake.
Ni msikivu.
Ni rafiki mkubwa wa Chivero.
Ni kiongozi bora.
Anafaa kuigwa na jamii



Nhamo

Ni kijana katika kijiji cha mtemi Masasa.
Ana majivuno na jeuri.
Hampendi Takadini kwani alimbagua kumpiga na hata kumdhalilisha.
Hafai kuigwa n ajamii.



Tendai

Mke mdogo wa mwisho wa mtemi Masasa.
Aliolewa bila kupenda, hakumpenda mtemi Masasa kwani alimzidi umri.
Alikuwa rafiki mzuri wa Sekai.
Ana mapenzi ya dhati kwa Takadini.
Ana bidii na mvumilivu.
Anafaa kuigwa na jamii



Nhariswa na mkewe

Ni wazazi wa Shingai
Wanashikilia mila desturi potofu
Hawakupenda kabisa kitendo cha mtoto wao kumpenda Takadini
Walimlazimisha kuolewa na Nhamo kwani walitaka sifa na maujiko
Walimtenga Shingai baada ya kutoroka na kuolewa na Takadini
Si wazazi wazuri
Hawafai kuigwa na jamii



Kutukwa

Ni mzee katika kijiji cha mtemi Masasa
Ni mpigaji mbira maarufu
Alimfundisha Takadini kupiga mbira
Alitoa mtazamo mbaya kwa wanakijiji wenzake kwa kuwaeleza sifa nzuri za Takadini
Alimpenda Takadini. Anafaa kuigwa na jamii




Mandhari



Mandhari aliyotumia Ben J Hanson ni mandhari ya kijijini kwani maisha ya watu na mazingira yanayoelezwa ni ya kijijini, masuala kama ya kilimo, ufugaji, sherehe za mavuno, makazi ya watu kukaa katika jumuiya ya pamoja kijamaa inayoongozwa na mtemi mmoja. Mfano mtemi Masasa, yote haya ni viashiria kuwa mandhari ni ya kijini. Mandahari ambayo mwandishi ameijengea mawazo yake na kuyaibua ni sadifu na halisi. Kwani maeneo ya vijijini ndiko kulikokithiri mambo ya imani potofu na za kishirikina kama vile kuwaua watoto Sope au albino.







Fani katika Riwaya ya Joka la Mdimu
Hakiki fani katika Riwaya ya Joka la Mdimu




MWANDISHI: ABDALLAH J. SAFARI



MCHAPISHAJI: HUDA PUBLISHERS



MWAKA: 2007




UTANGULIZI WA KITABU



Joka la mdimu ni riwaya iliyojengwa kwa visa tofauti tofauti vinavojengana kukamilisha masimulizi. Ni riwaya inayosawiri au kuakisi mambo yaliyopita ya nyakati za nyuma ambapo kulikuwa na shida kama vile za mafuta ya petroli, Nguo, vyakula nk. Pamoja na hayo zipo pia dhamira au mawazo ambayo yanasawiri maisha ya Mtanzania wa leo kama vile masuala ya rushwa na uhujumu uchumi.



Kwa upande wa fani ni riwaya ambayo mwandishi amewaumba vyema wahusika wake kwa kuwavika uhalisia vyema, amepanga visa vyake na amejitahidi kutumia lugha yenye mvuto na vionjo vya kisanaa huku akiwaburudisha wasomaji kwa mtindo wa kipekee.




JINA LAKITABU



Jina la kitabu limewekwa katika lugha ya picha, JOKA LA MDIMU ni nyoka anayeishi katika miti ya kijani. Nyoka huyu hupendelea kuishi katika miti ya Minyaa na Midimu inayofanana na rangi yake. Nyoka huyu awapo kwenye miti hiyo si rahisi kumtambua kutokana na rangi yake kufanana sana na miti hiyo. Hivyo ni nyoka hatari sana kwa binadamu.



Mwandishi anatumia taswira ya Joka la Mdimu kufananisha na viongozi ambao ni wananchi wenzetu, wanafanana na sisi, ni ndugu zetu damu yetu. Lakini ni hatari mno kwani hutugeuka na kuwa mafisadi, wala rushwa, hawatimizi majukumu yao, ni walaghai nk. Badala ya kusaidia wananchi wao hujali maslahi yao kwanza na hivyo kusababisha mifumo ya kiuchumi kuendelea kuwa migumu kwa wananchi na kupelekea kuongezeka kwa kiasi kikubwa cha watu walio maskini au hohehahe. Hivyo jina la kitabu linasawiri yaliyomo ndani ya kitabu na katika jamii.




MUUNDO



Riwaya ya Joka la Mdimu imetumia muundo changamani yaani kwa kiasi fulani ametumia rejea au rukia pia ametumia muundo sahili au msago.



Mfano ametumia muundo wa rejea katika sura ya Mindule ambapo anaanza kutueleza juu ya habari za Amani dereva wa taxi na adha anazopata kutokana na ukosefu wa mafuta na jinsi anavyoiendesha biashara yake hiyo. Lakini ndani ya sura hiyohiyo anaturudisha nyuma na kuanza kutuelezea namna Amani alivyopata kazi ya udereva Taxi na kutueleza juu ya mmiliki wa Taxi hiyo ambaye ni Shiraz Bhanj. Pia katika sura ya Boko anatueleza juu ya Safari ya Tino kwenda kumuona mwanae mgonjwa uk.73 ila hatuelezi inavyoendelea lakini anarukia kisa kingine cha Brown Kwacha na sura ya Kwale halafu badae anaturudisha nyuma na kuendelea kutuelezea juu ya habari za kuuguliwa kwa Cheche na Tino anapofika kumuona katika sura ya Dakta Makwati. Pia ametumia muundo wa moja kwa moja katika sura zingine kwani ameyapanga matukio yake katika usahili bila kuruka.



Pia mwandishi amegawanya visa na mtukio katika sura kumi ambapo kila sura ameipa jina kwa kutumia majina ya wahusika.

Sura ya kwanza, MINDULE: Hapa mwandishi anatueleza kuhusu habari za Amani dereva Taxi, masaibu anayopata katika kazi yake kutokana na uhaba wa mafuta katika vituo vya mafuta.
Sura ya pili, TINO: Hapa tunaelezwa kuhusu maisha ya Tino na kazi anazofanya ya kuvuta kwama. Tunaambiwa kuhusu hali ngumu ya maisha ya Tino na wakazi wengine wa Sega, hapa tunaelezwa pia kuhusu masuala ya uongozi jinsi ulivyo mbovu na ugawanywaji mbovu wa vyanzo vya uchumi na bidhaa.
Sura ya tatu, JINJA MALONI: Katika sura hii tunaelezwa kuhusu maisha ya Jinja Maloni, hapa anaibua dhamira kama vile za uvamizi, uhalifu na mauaji pia anaendela kutueleza kuhusu hali ngumu ya maisha.
Sura ya nne SEGA: Maisha ya wakazi wa Sega yanaelezewa hapa jinsi yalivyo ya dhiki, pia tunaelezwa kuhusu Tino na mkewe maisha yao yalivyo na familia yao, anaibua dhamira ya mapenzi ya dhati na upendo kwa familia.
Sura ya tano, BOKO: Hapa tunaelezwa kuhusu adha ya usafiri kwa watu, shida ya mafuta, ubovu wa miuondmbinu kama vile barabara, vinasemwa hapa.
Sura ya sita, BROWN KWACHA: Sura hii inaeleza habari za Brown maisha yake na tabia zake, anaibua dhamira kama vile uhujumu uchumi, biashara za magendo, suala la kutowajibika kwa watumishi, suala la kukosekana kwa uaminifu katika ndoa na mapenzi ya pesa ambapo sifa zote hizi alizibeba Kwacha.
Sura ya saba, KWALE: Hapa yanaelezwa mambo kuhusu hifadhi ya Kwale, safari ya Brown na Leila kwenda kutembea kwale. Hapa yanatajwa mambo ya udhalimu wa kuharibu mali za umma (maliasili za taifa) mfano pembe za ndovu, vipusa pia mapenzi yasiyo ya kweli.
Sura ya nane, DAKTA MIKWALA: Dakta Mikwala ndiye mhusika mkuu anayeelezwa hapa, tunalezwa juu ya ugumu wa upatikanaji wa huduma za afya kwani Cheche anashindwa kutibiwa kutokana na ukosefu wa fedha za kigeni.
Sura ya tisa, CHECHE: Tunaelezwa juu ya juhudi za Amani na Tino ili kumsaidia Cheche aweze kwenda kutibiwa Uingereza. Wanafanikiwa kupora benki na kupata pesa za kumtibu Cheche.
Sura ya kumi, MOTO: Hapa hatma ya visa vidogo vidogo imeelezwa kwa kutolewa hatma ya maisha ya Cheche na Brown Kwacha. Cheche alipata matibabu na kupona na Browna anafanikiwa kuirubuni serikali kwa kuipanga mahesabu ya uongo.




MTINDO



Mwandishi ametumia mitindo ya aina tofautitofauti ili kuweza kuipamba kazi yake ivutie.

Matumizi ya nafsi ya tatu Umoja. Imetawala: Mfano uk.5“Amani aliangalia…….” Uk.25 “Amani alijizuia” .Nafsi ya tatuwingi;mfano uk. 63 “wote walitoka nje kuelekea klabuni”.Pia uk.53 “wale wanaume walimvamia”
Matumizi ya nafsi ya pili: Mfano uk.106 “ mmechoka kuangalia video?” “aa tumeshaziona mara nyingi tunaombaainanyingine.” Mazungumzo baina ya mke wa Brown na wanae.Pia mazungumzo baina ya Brown na Leila.Uk.113. “habari za asubuhi”“ Nzuri sijui wewe” alijibu “Uliota njozi njema?” "Wapi?" "Kwa nini?"
Matumizi ya nafsi ya kwanza: Mfano uk. 39 “mimi nimemaliza” “….kuiba nimeiba sana….”
Matumizi ya nyimbo.Uk.70. wimbo wa Chaupele: “Chaupele mpenzi, haya usemayo Kama ni maradhi, yapeleke kwa Daktari Wanambia niache rumba,na mimi sikuzoea Sitaweza kuliacha rumba, kwa sababu yako Kama wanipenda, nenda kwa baba” Pia uk.58 “sega! Sega! Sega!, usioogope” wimbo waliouimba washabiki wa michezo.
Masimulizi ya hadithi ndani ya hadithi: Hapa mwandishi amemtumia muhusika kusimulia kisa kingine kidogo ndani ya kisa kikuu. Mfano uk.39 mhusika Tino anamsimulia mteja wake maisha yake ya mwanzo kabla hajaanza kazi ya kuvuta kwama.




MATUMIZI YA LUGHA



Mwandishi A. Safari ametumia lugha fasaha na inayoeleweka kwa wasomaji wake. Kuna matumizi ya lugha nyinginezo kama vile kiingereza.Uk.55 “city devils” uk.155 “I miss my family”, uk.24 “Hey man you will pay extra money”, uk.99 consignment”.Pia kuna matumizi ya lugha ya kiarabu, mfanouk.45 “Salaam aleikum mayitun” uk.42 “Inna Ilayhi Raajiunna!”, uk.13, “Insha Allah!”. Vilevile kuna matumizi ya lugha ya mtaani uk.39 “msela”, “ndito”, “kashkash”.




Matumizi ya tamathali za semi.

Tashibiha: Uk.117 “ngozi yake nyeusi kama udongo wa mfinyanzi”Uk.122 “mweusi kama sizi la chungu”Uk.9 “Zepher 6 ile iliunguruma kama simba dume”Uk.10 “mteuzi mithili ya Mbega”Uk.35 “……miguu yake ikakazana mithili ya upinde uliotaka kufyatuliwa”
Sitiari: Uk.91 “Brown Kwacha alikuwa kinyonga”Uk.15 “sarahange wetu mboga kweli siku hizi”Uk.40 “huku twakaa vinyama vya mwitu” Uk.72 “sote ni kobe”
Tashihisi: Uk.109 “……gari lile zuri lilioondoka kwa madaha” Uk.143 “ kuta nyeusi za nyumba zaidi ya kumi zilisimama twe!kuomboleza” Uk.91 “pua zake zikalakiwa na riha na ashrafu ya manukato”;Uk.12 “utumbo ulimlaumu”; Uk.27 “mvua ikapiga kwa kiburi na kuviadhibu vibati vibovu”.
Tafsida: Uk. 49 “isijekuwa nimekukatiza haja!”,pia uk. huohuo“kinyesi”.




Mbinu nyingine za kisanaa.

Takriri: Uk.151 “mwizi! Mwizi! Jambazi! Jambazi!”Uk.57 “shinda! Shinda! Shinda!”Uk.33 “karibu baba, kariibu kaka, karibu mkwe” Uk.72 “uhuru upi? Uhuru gani? Uhuru wa nini na nani?”
Mdokezo: Uk.149 “lakini……..”
Onomatopea au tanakali sauti: Uk. 1 “saa mezani niliendelea kugonga taratibu ta! ta! ta!”; Uk.10 “ikatoka sauti kali tupu ta nye nye”;Uk.67 “upepo wa stova uliolia shshsh”;
Tashtiti: Uk.113. leila anamuuliza Brown maswali ambayo anayajua majibu yake. Brown:“uliota njozi njema? Leila: Wapi?” Leila:Kwanini? Brown:Mwenywe unajua”
Nidaa: Uk.39 “Aaa! Limbukeni wa jiji anataka kunitia kashkash”: Uk 30 “nguo zangu Mungu wee!” Uk.42 “Inna Lillah wa Inna Ilayhi Raajiunna!” Uk.92 “Ah! Leila kwacha alimsalimia kwa furaha” Uk. 105 “Lahaula”




Matumizi ya Semi.

Methali: Uk.78 “asilojua mtu ni usiku wa kiza”Uk.83 “ukiona mwenzako anyolewa zako tia maji”Uk.98 “mtaka waridi sharti avumilie miiba”Uk. 99 “biashara haigombi”Uk.43 “ajizi nuksani huzaa mwana kisirani”
Misemo: Uk.10 “asiye na bahati habahatishi”Uk.47. “asiyezika hazikwi”Uk.64 “mmetupa Jongoo na mtiwe”Uk.98 “asali haichomvwi umoja”Uk.111 “ajali haina kinga”Uk.115 “mwenye macho haambiwi tazama”Uk.120 “matendo hushinda maneno”Uk.47. “asiyezika hazikwi”
Nahau: Uk.11 “sio unanilalia kila mara” –kunidhulumuUk.107 “alikonda akajipa moyo” –kujifariji moyo




Matumizi ya taswira



Taswira mwonekano imetumika, ambayo inatujengea picha kutokana na vitu tunavyovifahamu. Mfano uk.76 “alisema kijana mmoja wa kiume kavaa sketi, blauzi na sidiria iliyopachikwa juu yake. Kichwani alifunga kilemba.”Hii inatupa picha halisi ya huyo kaka kwani tunaposoma ni kama kweli tunamuona kutokana na jinsi mwandishi alivyoelezea. Pia uk.135 “mwambie yule jamaa pale atayarishe kuku mzuri wa kukaanga ”……… na kachumbari yenye pilipili” hii inamfanya msomaji ahisi ladha ya kuku na hiyo pilipili kwa maneno ambayo mwandishi ameyajengea taswira na hii ni taswira hisi.



Joka lamdimu ni taswira ya nyoka mbaya ambaye amefananishwa na viongozi wabaya.






WAHUSIKA



AMANI

Ni dereva taxi
Ana upendo wa dhati
Ni mchapakazi
Ana hekima na busara
Ana huruma
Ni rafiki wa kweli wa Tino
Kutokana na hizo sifa amani ni mhusika bapa
Anafaa kuigwa na jamii



TINO (mhusikabapa)

Ni mchapakzi
Mlezi bora wa familia
Baba wa Cheche
Ana huruma
Ana upendo wa dhati
Ni makini
Ni jasiri
Ni mwanamichezo
Anafaa kuigwa na jamii



BROWN KWACHA

Ni mkurugenzi wa idara ya fedha za kigeni
Ni muhuni na Malaya
Fisadi na mla rushwa
Anafanya biashara haramu
Hana mapenzi kwa familia yake
Anapenda anasa
Si muaminifu kwa mkewe
Si muadilifu
Hafai kuigwa na jamii
Ni mhusika bapa



JINJA MALONI

Ni jasiri na mwenye nguvu
Ana huruma na upendo
Mchapakazi
Mlevi
Maskini
Ni mhusika duara



DAKTARI MIKWALA

Ni daktari bingwa wa mifupa
Anapenda rushwa
Si muwajibikaji katika kazi yake
Ni mlevi
Hafai kuigwa na jamii
Ni mhusika bapa



SHIRAZ BHANJ

Ni mfanyabiashara
Ni mtoa rushwa
Ana biashara za magendo
Rafiki wa Brown
Hafai kuigwa na jamii
Ni mhusika bapa



ZITTO

Ni mfanyakazi bandarini
Ni mwanamichezo
Ni jasiri ana kipato duni
Rafiki wa Tino na Aman



CHECHE

Ni mtoto wa Tino
Ana nidhamu na bidii
Ni mwanamichezo
Ana upendo kwa wazazi wake
Ni mtiifu na msikivu
Mcheshi na mudadisi
Alivunjika kiuno michezoni
Ni mhusika bapa



MWEMA

Ni mke wa Tino
Mvumilivu
Ana mapendo ya dhati kwa familia yake
Ni mchapakazi
Ni mhusika bapa



JOSEPHINE NA LEILA

Wasichana wahuni waliojiuza kwa Brown Kwacha
Hawafai kuigwa na jamii




MANDHARI



Mandhari aliyoitumia mwandishi ni ya mjini, anataja baadhi ya maeneo ya nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam kama vile Boko, Sega, Mindule. Mandhari hii ni sadifu kwa yale ambayo mwandishi ameyaeleza kwani masuala ya rushwa, upotevu wa haki, hali ngumu ya uchumi na maisha kwa ujumla, ni matatizo halisi ya jamii ya Tanzania.



Uhakiki wa Fani katika Tamthiliya




Fani katika Tamthiliya ya Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe



JINA LA KITABU: NGOSWE PENZI KITOVU CHA UZEMBE



MWANDISHI: EDWIN SEMZABA



WACHAPISHAJI: NYAMBARI NYANGWINE PUBLISHERS



MWAKA:2006



UTANGULIZI WA KITABU



Ngoswe penzi kitovu cha uzembe ni tamthiliya maarufu sana ambayo imewahi kuigizwa katika redio Tanzania na katika majukwaa mbalimbali hapa nchini. Ni tamthiliya ambayo imeundwa vyema katika vipengele vya fani na maudhui. Ameteua lugha nzuri na yenye mvuto kwa wasomaji yenye mbinu za kifasihi zilizosheheni, muundo wenye mtiririko mzuri, unaoakisi kuanza kuchipuka kwa matukio mpaka kilele cha matukio. Wahusika wamebeba vyema uhusika wao mfano Ngoswe.



Ameibua dhamira kuhusu mambo yanayoigusa jamii ya leo kama vile uzembe, madhara ya ulevi, uzembe kazini, suala la matabaka kati ya mjini na vijijini. Mtazamo, falsafa na msimamo wake ni kulenga kuibadilisha jamii na kuleta maendeleo.



JINA LA KITABU



Jina la kitabu “Ngoswe penzi kitovu cha uzembe” ni jina ambalo limesawiri vyema yaliyomo ndani ya kitabu hicho, kwani Ngoswe ndio jina la mhusika mkuu anayebeba dhamira kuu ya tamthiliya. Pia penzi limeonekana kuwa ni kitovu cha uzembe kwani ndio yaliyopelekea kuteketezwa kwa karatasi za takwimu za sensa. Hivyo jina la kitabu si tu kwamba limesawiri yaliyomo katika kitabu bali pia katika jamii.



MTINDO



Mtindo alioutumia mwandishi ni dayalojia au majibizano. Mwandishi amepanga visa na masimulizi kwa kutumia majibizano ya wahusika.

Matumizi ya nafsi ya kwanza.Mwandishi ndiye ameyafafanua na kuelezea baadhi ya matukio. Katika karibu kurasa zote mwandishi ameonekana kuwa ndiye msimuliaji wa matukio.
Matumizi ya nafsi ya pili.Hapa watu wawili na zaidi wanajibizana. Tamthilya hii wahusika wanaojibizana kuibua dhamira na migogoro. Kuna majibizano baina ya mzee Mitomingi, Ngoswe na Mazoea nk.unaweza kupata mfano uk. wowote kwani ndio mtindo uliotawala.



MUUNDO



Muundo uliotumika ni muundo wa mojakwamoja au sahili. Kwani ameonesha tangu mwanzo wa mambo mpaka mwisho, anajenga visa vidogo mpaka visa vikuu au kileleni.Amepanga visa na matukio yake katika maonesho matano. Kila kichwa kina maelezo yaliyojadiliwa katika onesho hilo.

KIJITO: Hapa yanaeleza jinsi mambo yanavyoanza. Jinsi Ngoswe anavyoingia kijijini anavyopokelewa na kuanza kufahamiana na wenyeji wake.
VIJITO: Hapa Ngoswe anaanza kufanya kazi iliyompeleka kijijini na tunaanza kuoneshwa changamoto anazokumbana nazo.
MTO: Ni mwendelezo wa matukio ya mwanzo hapa visa vinazidi kukua.
JITO: Hapa Ngoswe anakumbana na changamoto nyingi zaidi katika kazi yake. Na hapa anazidi kuanguka kwani anajiingiza katika mapenzi na msichana Mazoea, anaendekeza ulevi na kuharibu kazi kabisa.
BAHARINI: Hapa inaoneshwa mwisho wa mambo jinsi yalivyokuwa. Yanaonekana mahojiano baina ya Serikali na Ngoswe na Mitomingi juu ya uzembe uliofanyika wa kupoteza takwimu na hapa ndipo suluhisho linapotolewa juu ya matatizo hayo.



WAHUSIKA



NGOSWE

Kijana wa kiume umri kati ya miaka 20-25
Ameelimika na amestaarabika
Anatumwa na serikali kufanya sensa kijijini
Anajihusisha na mapenzi na msichana mazoea
Ni mlevi
Hana umakini katika kazi
Aliharibu kazi ya serikali
Hafai kuigwa na jamii



MAZOEA

Ni msichana mwenye umri kati ya miaka 18-20
Ni binti wa Mzee Ngengemkeni Mitomingi
Hana elimu na hajastaarabika
Ana nidhamu ya woga
Ana tama
Hana msimamo alikubali kuchukuliwa na Ngoswe hali akijua alishatolewa mahari
Hafai kuigwa na jamii.



NGENGEMKENI MITOMINGI

Ni balozi katika kijiji chake
Ni baba mzazi wa Mazoea
Ameoa ndoa ya mitara, ana wake wawili
Hajaelimika
Anashikilia mila na desturi za kale
Mlevi
Mkali sana
Anateketeza karatasi za takwimu



MZEE JIMBI

Mwanakijiji
Hajaelimika kwani hajui hata umri wake
Ni mlevi
Ana wake wawili
Anashikilia ukale



MAMA MAZOEA

Mke mkubwa wa Mitomingi
Mama yake Mazoea
Mlezi wa familia
Hapewi nafasi ya kutoa maamuzi katika familia



MAMA INDA

Mke wa pili Mzee Mitomingi
Mama yake Huzuni
Hapewi nafasi ya kutoa maamuzi
Ni mlezi wa familia.



MANDHARI



Mandhari ya tamthiliya hii imechorwa katika mazingira ya kijijini. Mambo yanayoelezwa ni ya kijijini mfano kilimo, hali ya watu kimaisha, huduma duni sana za kijamii kama vile shule, umbali wa makazi toka nyumba moja hadi nyingine. Haya yanatudhihirishia vyema mandhari hiyo ambayo kwayo imeibua dhamira mbalimbali kama vile umaskini, ukosefu wa elimu, huduma duni za afya vijijini, masuala ya imani potofu nk.



MATUMIZI YA LUGHA



Lugha aliyotumia mwandishi ni lugha fasaha na rahisi kueleweka kwa wasomaji. Pia kuna matumizi ya lugha nyingine mfano uk. 1 “bell bottom”



Matumizi ya semi

Methali:Uk.22 “Penye nia pana njia”.Uk.27 “Waona vyaelea vyaundwa.”
Misemo:Uk.14 “Akuwaniae ujovu haji kweupe”
Nahau:Uk.11 “hebu keti tutupe mawe pangoni” –tule chakulaUk.7 “mbongo zimelala”-ana maarifa Uk.14 “pombe na yeye ni pete na chanda”- anapenda pombe sana.



Matumizi ya tamathali za semi

Tafsida: Uk.21 “Wala hajarudi, kama ingekuwa ni kujisaidia si angekuwa amekwishamaliza?”
Tashbiha: Uk.1 “vumbi jekundu kama ugoro wa subiana”Uk.8 “sarawili yake miguuni kama kengele ya bomani”Uk.17 “wanaondoka huku wakitazamwa kama vile mizuka”
Sitiari: Uk.7 Mama Mazoea : “kiziwi mkubwa wee!”Uk.14 “pombe na yeye ni pete na chanda!”Uk.26. “karatasi? za takwimu? Ndio wanyama gani hao?”
Mubaalagha: Uk.11 Mama Mazoea : “kupeleka chakula ndio umefanya makao!”Mama mazoea : “Kujibu swali ndio ukachukua mwaka mzima!”



Mbinu nyingine za kisanaa

Mdokezo: Uk.22 Mazoea : “sijui….. siwezi….. namuogopa baba”Uk.16 Ngoswe : “huyo mtoto wenu wa kwanza anaishi hapa au…..”
Takriri: Uk.9 “Mama Masikio! We Mama Masikio!”Uk.13. “Hodi! Hodi!”Uk.2 “karibu karibu”
Tashtiti: Uk.5 Ngoswe: “hivyo waitwa nani?”Mazoea: “mie?”Uk.22 Ngoswe: “mchumba? Kwani mchumba ni kitu gani?”Uk.26 Mitomingi: “karatasi? Za takwimu? Ndio wanyama gani hao?Hapa wahusika waliuliza maswali ambayo majibu yake waliyaelewa ila kutokana na kutaka kudhihirisha hasira, msisitizo nk. Ndio maana wametumia tashtiti.
Onomatopea/tanakali sauti: Uk.7 Kifaruhande anacheka “Ha! ha! ha!



Ujenzi wa taswira



Mwandishi ametumia taswira ya mto kuelezea visa vyake. Sehemu ya kwanza ni sehemu ya kijito, kijito ni kimto kidigo mwandishi hapa anaanza kueleza mambo yakiwa machanga kabisa ndio yanaanza.



Sehemu ya pili ni vijito. Huu ni muunganiko wa vijito vidogovidogo hapa mwandishi anaanza kueleza visa vidogovidogo. Sehemu inayofuata ni sehemu ya Mto. Hii inaashiria mambo yameanza kuwa mazito, visa vinakua zaidi na Ngoswe anazidi kuingia katika changamoto kubwa zaidi.



Pia Jito ni taswira ambayo mwandishi ameitumia kuashiria hatari zaidi mambo makubwa zaidi na hapa ndipo tunaona Ngoswe anaanguka kabisa katika kazi yake kwani Jito ni lenye maji mengi na yanayoenda kwa kasi hivyo huhitaji umakini mkubwa zaidi.



Mwisho sehemu ya Bahari ambapo hapa ndipo hatima ya mambo inaelezwa Ngoswe anazama na kupotea kabisa! Hafanikiwi kutoa takwimu kwani karatasi zilichomwa moto.






Fani katika Tamthiliya ya Kilio Chetu





MWANDISHI: MEDICAL AID FOUNDATION



WACHAPISHAJI: TANZANIA PUBLISHING HOUSE (TPH)



MWAKA: 1996




JINA LA KITABU



KILIO CHETU ni jina ambalo linaasadifu yaliyomo katika kitabu. Masuala yanayotajwa mule kama vile upotofu wa maadili kwa vijana wadogo kama Suzi na Joti, suala la mimba za utotoni, madhara ya gonjwa hatari la UKIMWI kwa jamii kweli ni kilio chetu ni kilio cha Taifa zima. Kwani katika mambo yanayoiyumbisha jamii kimaendeleo ni upotovu wa maaadili.



Jina hili ni sadifu katika jamii. Mwandishi amelitumia wakati muafaka kabisa kwani mambo anayoyaeleza ndio changamoto katika jamii ya leo. Hivyo kupitia hili jamii si budi kubadilika.




UTANGULIZI WA KITABU



Kilio chetu ni tamthiliya ambayo imejieleza vyema katika fani na maudhui. Tamthiliya hii inamuhusu mhusika Suzi na Joti ambao ni watoto wadogo sana. Wanajiingiza katika mapenzi katika umri mdogo kutokana na ukosefu wa elimu ya kijinsia. Inatueleza kuhusu athari za ugonjwa huu usiobagua. Pia tunafahamishwa kuhusu mtazamo wa wazazi na walezi kuhusu utoaji wa elimu ya jinsia kwa vijana wao. Wapo wanaolipokea kwa mtazamo chanya na wengine hasi.



Kwa ujumla ni tamthiliya nzuri kwani ina mtazamo wa kimabadiliko unaolenga kuwakomboa vijana wetu kutoka katika janga la ugonjwa hatari wa UKIMWI.




MUUNDO

Sehemu ya kwanza: Inaonesha jinsi gonjwa la UKIMWI linavyoikumba jamii. Mwandishi anaeleza kuhusu Dubwana linaloikumba jamii.
Sehemu ya pili: Mwandishi anaeleza kuhusu athari za UKIMWI, jambo ambalo lilipelekea kifo cha Fausta. Pia Suzi agundulika kujihusisha na mapenzi baada ya kukutwa na vidonge vya kuzuia mimba.
Sehemu ya tatu: Inaeleza juu ya watoto ambao wameshajiingiza katika suala la mapenzi licha ya kuwa na umri mdogo mfano ni Joti na Suzi. Pia madhara ya utandawazi yanaelezwa hapa mfano kuoneshwa kwa picha za ngono.
Sehemu ya nne:Tunaelezwa juu ya tabia hatarishi za Joti za kuwa na mahusiano na wasichana wengi mfano Chausiku, Yoranda, Gelda na Suzi. Hapa Joti anafanikiwa kumrubuni tena Suzi. Pia tunaoneshwa jinsi Ana anavopingana na vishawishi kutokana na kupata elimu ya jinsia.
Sehemu ya tano: Suzi anagundulika kuwa na mimba ya Joti, anajutia kosa hilo anajilaumu sana.
Sehemu ya sita: Inatuonesha jinsi Joti alivyokuwa magonjwa tayari kutokana na UKIMWI. Hapa ushauri mzuri unatolewa kuhusu namna ya kumtunza mgonjwa wa UKIMWI na kumfanya aishi kwa matumaini. Hapa mwandishi anapinga mila potofu kuhusu UKIMWI kuwa si kurogwa bali ni ugonjwa unaoambukizwa.




MTINDO



Tamthiliya hii imesheheni katika mitindo kadha wa kadha inayopamba kazi hii. Mtindo uliotumika ni dayalojia au majibizano.



Mwandishi ametumia mtindo wa mianzo na miisho ya kifomula ya usimulizi ambao ni mtindo wa usimulizi wa fasihi ya kiafrika. Mfano uk.1 mwandishi anasema “paukwa….. pakawaa…. Niendelee…. nisiendelee? ….. au mmechoka? Uk.113,pia uk.36 mwandishi anasema “na hadithi yangu imeishia hapo”.Pia mwandishi ametumia mtindo wa utambaji kwani ndiye anayesimulia na kuelezea matukio.




Matumizi ya nafsi



Nafsi ya pili ndiyo iliyotawala, mwandishi ametumia majibizano ya watu wawili mfano Suzi na Joti, pia watu watatu n.k.Pia mwandishi ametumia tanzu nyingine za fasihi mfano wimbo uk.27




Wahusika



SUZI

Ni binti mdogo wa darasa la sita
Anajihusisha na mapenzi na Joti
Hana msimamo
Anapata mimba katika umri mdogo
Ana hatari ya kuwa na UKIMWI
Hakupewa elimu ya jinsia
Ana tamaa kwani alitamani vitu alivyohongwa na Joti.
Hafai kuigwa na jamii tutokana na tabia zake au sifa zake



JOTI

Ni kijana mdogo wa kiume
Ana mahusianao ya mapenzi na wasichana wengi Suzi, Gelda, Yoranda na Chausiku
Hana elimu ya jinsia
Ana makundi mabaya ya marafiki
Anaathirika na kufa kwa gonjwa la UKIMWI
Amechangia kuharibu maisha ya Suzi kwa kumrubuni
Ni mlaghai
Hafai kuigwa na jamii



MAMA SUZI

Ni mzazi wa Suzi
Anashikilia ukale hataki mabadiliko
Hampi mwanae elimu ya jinsia
Alichangia kuharibu maisha ya Suzi
Ni mkali sana katika malezi hatumii busara bali hasira
Hafai kuigwa na jamii



BABA JOTI

Ni mzazi wa Joti
Hayupo tayari kutoa elimua ya jinsia
Anashikilia ukale
Ni mkali anatumia viboko kuelimisha jambo ambalo si sahihi
Amechangia kuharibu maisha ya Joti
Ni muhuni, si muaminifu katika ndoa yake
Hafai kuigwa na jamii



ANNA

Ni binti mdogo wa shule
Ana elimu ya jinsia
Ana msimamo mzuri anashinda vishawishi
Anatoa elimu kwa vijana wenzake kuhusu athari za kujiingiza katika mapenzi katika umri mdogo
Ana tabia njema
Hana tama
Anafaa kuigwa na jamii.



BABA ANNA

Ni mzazi wa Anna
Anatoa elimu ya jinsia kwa wazazi na watoto
Ni mlezi bora
Alichangia maisha ya Anna kuwa ya mafanikio
Anafaa kuigwa na jamii



MJOMBA

Ni kaka yake Mama Suzi
Anaendana na wakati wa sasa
Anatoa elimu ya jinsia kwa vijana na wazazi
Ni mlezi bora ni mshauri bora
Anatoa elimu ya UKIMWI kwa Baba Joti anapinga mila potofu
Anafaa kuigwa na jamii



MAMA JOTI

Mzazi wa Joti
Ndoa yake ipo matatani kuingiliwa na mke mwingine
Anaelewa kuwa jamii imebadilika na wazazi wanapaswa kuwaelimisha watoto



JIRANI

Ni jirani wa Baba Joti
Ana imani potofu za kishirikina, anaamini Joti alilogwa
Haamini kuwa UKIMWI upo



CHAUSIKU

Ni msichana wa mtaani
Mfanyabiashara wa vitumbua
Ni jirani wa Suzi
Ana tabia mbaya ni muhuni
Alichangia kuharibu maisha ya Joti
Ana mahusiano ya kimpenzi na vijana wadogo mfano Joti na watu wazima pia, mfano Mpemba.




CHOGO, MWARAMI NA JUMBE

Ni marafiki wa Joti
Ni wanafunzi wadogo
Si marafiki wazuri
Wana tabia mbaya wanashauriana kuhusu mambo mabaya
Hawafai kuigwa na jamii




MANDHARI



Mandhari ni sehemu / mahali / mazingira ambayo ni matukio ya hadithi au masimulizi hutendeka /hufanyika /hutokea.



Mandhari huweza kuwa halisi ikijumuisha mazingira yanayoweza kudhihirika katika ukawaida na pia mandhari yaweza kuwa ya kubuni ikiwa haina uhalisia, katika tamthilia hii tunaweza kusema mwandishi ametumia mazingira ya uhalisia kutokanana mandhari zifuatazo;

Mandhari ya shule,kwa upande wa joti na suzi kuanzia sehemu ya kwanza,
Mandhari ya nyumbani na mtaani uk 12



Mandhari aliyoitumia mwandishi ni ya mjini, hii ni kutokana na maelezo ya mhusika jirani anaposemauk.32 “……mie toka siku ile nimwone hospitali sijakaa mjini. Nilikwenda zangu shamba kupambana na Nyani wala nafaka.”Pia lugha ya mtaani iliyotumiwa na vijana Joti, Mwarami na wenzake, masuala ya picha ya “X” yaani viashiria vya mambo ya mjini kwani yamekithiri sana mijini. Maeneo yanayotajwa kama vile uwanja wa Sabasaba ni uwanja uliopo mjini, masuala ya lifti kwa wasichana hasa wanafunzi yapo mijini. Mfano.uk.27 pia kuna mandhari ya nyumbani na mtaani.



Mandhari aliyotumia mwandishi inasawiri maudhui yake katika jamii. Kwani anaibua mambo yaliyo katika jamii.




MATUMZI YA LUGHA



Lugha iliyotumika ni lugha iliyo na ubunifu wa kipekee wenye mvuto wa kisanaa. Lugha ni rahisi na inayoeleweka vyema kwa hadhira lengwa. Pia kuna matumizi ya lugha nyingine mfano kiingereza na lugha za kikabila. Kiingereza mfanouk.21 “tuition” uk.16 “come”.Lugha za kikabila mfano wimbo uk.35“Joti afitwe sanda salauya; Ena ena salauya …………………….”




Matumizi ya lugha ya mtaani



Mfano uk.16 “mshefa” “mshikaji”-rafiki.Uk.17 “kamba” kudanganya jambo;Uk.22 “vidosho”wasichana;Uk.16 “kanitolea nje” kukataa jambo fulani.




Matumizi ya tamathali za semi

Tashibiha: Uk.1 “wakapukutika kama majani”Uk.5 “mgumu kama mpingo”Uk.6 “miti inaungua kama mabua”Uk.13 “Dubwana limetanda kama utando wa Buibui”
Tashihisi: Uk.2 “vifo vikawazoa”kifo huua tu lakini kimepewa uwezo wa kuzoa
Sitiari: Uk.8 “We Mbwa mweusi”Uk.9 “Nyoka wee”Uk.21 “huyo kinyago wako anakimbia nini?”
Tafsida: Uk.4 “kafa kwa kukanyaga nyaya”– kafa kwa UKIMWI
Mubaalagha: Uk.4 “Mtu si mtu, kizuka si kizuka”




Matumizi ya mbinu nyingine za kisanaa

Tanakali sauti/ Onomatopea: Uk. Joti akasema“….acha moyo unipwite “Pwi! Pwi! Pwi!”Uk.25 “….hebu nitolee uchafu wako mie ptuu!”
Tashtiti: Uk.15 “….huyu ni Suzi kweli au nani?”Uk.36 “kwanini Joti……… kwanini Joti afe?”
Takriri: Uk.1 “watu wakapukutika, wakapukutika…..” “tunakwisha, tunakwisha”Uk.2 “vifo vikawzoa, vikawazoa .…. vikawazoa”Uk.16 “piga domo, piga domo”




Matumizi ya semi

Methali: Uk.6 “wembamba wa Reli Treni inapita”Uk.11 “mzazi usipomfunza walimwengu watamfundisha”Uk.19 “shukrani ya Punda ni mateke”Uk.24 ‘Ndege mjanja ananaswa na tundu bovu”
Nahau: Uk.6 “nimekuvulia kofia”-nakuheshimuUk.21 “anajigongagonga” –anajipendekeza
Misemo: Uk.4 “kuwa nyumanyuma kama koti”Uk.6 “kifua simkingii maana siwi naye”Uk.7 “makapera kibao Mume wangu wa nini?”Uk.22 “mapenzi ni tiba”Uk.26 “…..unakimbilia suti na nepi hujavaa”




Matumizi ya taswira



UK.1 “dubwana” ugonjwa wa UKIMWI;Uk.7 “Nguru” aina ya Samaki wabaya–amefananishwa na mtu mbaya;Uk.21 “kinyago” Suzi.





Fani katika Tamthiliya ya Orodha






JINA LA KITABU



Jina la kitabu ORODHA ni sadifu kwa yaliyomo. Katika kitabu inatajwa orodha ya mambo ambayo yanaweza kusaidia kuepusha UKIMWI. Orodha hii inatolewa na mhusika Furaha ambaye aliomba isomwe katika mazishi yake. Mambo hayo au orodha hiyo ni pamoja na uwazi, ukweli, uadilifu, matumizi ya kondom, uelewa, upendo, elimu, uwajibikaji na msamaha. Mwandishi anaona kuwa endapo mambo haya yatazingatiwa hakika tutapunguza maambukizi zaidi ya virusi vya UKIMWI.




UTANGULIZI



Tamthiliya ya Orodha ni tamthiliya inayohusu suala zima la ugonjwa wa UKIMWI na madhara yake katika jamii. Mwandishi anaweka wazi kuhusu gonjwa hili. Mhusika mkuu Furaha anaathirika na gonjwa hili na kufariki dunia. Kimaudhui tamthiliya hii imesawiri maisha ya sasa ya jamii ya Watanzania kwani ugonjwa huu bado ni tishio. Kwa upande wa fani, mwandishi amewaumba vyema wahusika wake, muundo wake ni unaomvutia msomaji kujua ni nini kingeendelea mbeleni, ameteua lugha nzuri ya kisanaa. Haya yote yanajielekeza katika uchambuzi tutaoenda kuufanya.




MUUNDO



Mwandishi ametumia muundo changamano kwani katika sehemu ya 1 na 2 anatuonesha mazishini ambapo yanafanyika mazishi ya Furaha. Sehemu ya 3-20 anaanza kutuelezea juu ya maisha ya Furaha mpaka kifo chake ambao huu ni msago au muundo sahili. Halafu sehemu ya 17-19 na ishirini 20 anatuonesha juu ya mzozo wa orodha na hatma ya mazishi ya Furaha.



Mwandishi ameweka kazi yake katika onyesho moja. Na katika onyesho hilo ameweka sehemu ndogondogo ishirini zinazojengana kukamilisha tamthiliya nzima.

Sehemu ya kwanza: Inaanza kwa kuonesha vifani vinne vimeganda kifani cha kwanza, wahusika wameganda katika mikao inayotambulisha wasifu wa wahusika. Kifani cha pili kinaonesha wagonjwa wakiwa katika mateso. Kifani cha tatu kinaonesha wagonjwa wakiwa katika maumivu makali sana.
Sehemu ya pili: Hapa inaelezwa juu ya siku ya msiba wa Furaha. Mama yake Furaha anaeleza watu kuwa Furaha aliacha orodha ambayo alitaka isomwe hadharani katika mazishi yake. Suala hili linazua mgogoro na hofu kuu kwa watu. Padre James anaweka juhudi kuzuia barua isisomwe.
Sehemu ya tatu: Sehemu hii tunaoneshwa juu ya maisha ya Furaha nyumbani kwao, baba na mama yake na wadogo zake. Baba yake anaonekana kutofurahishwa na mwenendo wa Furaha kwani anamkanya kwa maneno makali ya laana. Kama vile hatopata mtu wa kumuoa. Anamuasa Furaha kuonesha mfano mzuri kwa wadogo zake.
Sehemu ya nne: Hapa Furaha kwa mara ya kwanza anatoroka nyumbani kwao usiku wa manane pamoja na Mery kwenda baa. Mdogo wake anabaini kitendo hicho na kutishia kushitaki kwa wazazi lakini Furaha anamtishia kumchinja.
Sehemu ya tano: Wanaonekana Mery na Furaha wako baa wakinywa pombe na kucheza na wanaume. Hapa Furaha anajifunza mambo mapya mabaya kama vile ulevi kupitia rafiki yake Mery. Pia anaanza mahusiano ya mapenzi na wanaume mfano Bw. Ecko.
Sehemu ya sita: Hapa Furaha anamwendea Padre James kwa ajili ya maungamo kwani alikunywa pombe na kulala na wanaume, lakini Padre James anamwambia Furaha aende kesho yake katika chumba chake cha kujisomea nyuma ya kanisa na taa zitakuwa zimezimwa kuficha utambulisho. Na hapa ndipo Furaha anapozini na Padre kwani Padre alishikwa na tamaa.
Sehemu ya saba: Baba na Mama Furaha wanamkanya Furaha kuhusu tabia yake ya umalaya na ulevi. Furaha anaomba msamaha.
Sehemu ya nane: Furaha anakutana na Kitunda aendapo sokoni, katumwa na mama yake. Lakini anamkuta Kitunda akisikiliza mziki Furaha anashawishika, Kitunda anamshawishi zaidi na hata avute bangi ila hakubali. Pia wanazungumzia juu ya jiji la Dar es Salaam. Habari hizo zinampagawisha Furaha na kutamani sana aende.
Sehemu ya tisa: Salim anarudi toka masomoni Dar es Salaam. Anaonana na mpenzi wake wa zamani Furaha. Wanasalimiana kwa hamu na furaha tele.
Sehemu ya kumi: Salim na Furaha wanakutana na kuelezana habari za kitambo kwani walitengana kwa muda mrefu, wanapanga mipango juu ya mahusiano yao.
Sehemu ya kumi na moja: Wanakijiji wanazungumzia juu ya tabia ya umalaya ya Furaha, pia wanazungumzia juu ya mahusiano ya Furaha na Salim. Hawapendezwi na tabia ya Furaha na kuamua kumtaarifu mama yake.
Sehemu ya kumi na mbili: Mama Furaha anachukua jukumu la kumhoji mwanae juu ya tabia yake. Furaha hakubaliani na lolote. Hali ya Furaha inaanza kudhoofu na mama yake anaaingiwa hofu.
Sehemu ya kumi na tatu: Furaha yupo sebuleni akisali. Baba yake anamuonya zaidi na kumshauri aolewe na Salim kwani ni kijana mzuri anayefaa.
Sehemu ya kumi na nne: Hapa hali ya Furaha inazidi kutetereka, anachukuliwa vipimo vya damu na kugundulika kuwa ana virusi vya UKIMWI. Hali hii inamshitua sana mama yake. Anamuhoji kama aliwahi kutembea na mwanaume yeyote, anamueleza njia za upataji wa UKIMWI na Furaha naanza kulia kwa kutambua kosa lake.
Sehemu ya kumi na tano: Wanakijiji wanapata habari juu ya kuumwa kwa Furaha na wanazieneza. Juma, Kitunda, Padre James, Salim, Bw. Ecko wanapata pia habari hizi. Wanaingiwa na hofu kubwa endapo watakuwa wameambukizwa UKIMWI au majina yao yamo kwenye orodha?
Sehemu ya kumi na sita: Salim anaamua kumtembelea Furaha nyumbani. Akiwa katika hali mbaya sana ya ugonjwa Furaha anamuweka wazi Salim juu ya kuathirika kwake kwa UKIMWI. Salim anaingiwa hofu anamuomba Furaha barua yenye orodha kwa shauku lakini hampatii. Hali hii inamuudhi Salim. Na hapa ndipo Furaha anapokata roho!
Sehemu ya kumi na saba: Hapa tunaelezwa juu ya juhudi za Bw. Ecko, na Juma za kutaka kuiba barua yenye orodha katika chumba alicholazwa maiti ya Furaha. Lakini hawafanikiwi. Familia ya Furaha wanaamini kuwa kuna mizimu katika chumba cha maiti kutokana na kelele za Juma na Bw. Ecko, na Kitunda.
Sehemu ya kumi na nane: Padre James anaomba kusomewa barua hiyo kabla ya mazishi lakini mama furaha anakataa. Anaamua kuitafuta mwenyewe sebuleni bila mafanikio.
Sehemu ya kumi na tisa: Asubuhi siku ya mazishi. Ecko, Juma na Salim wanaonekana wakitafuta suluhu ya namna ya kuzuia orodha isisomwe ila hawafanikiwi.
Sehemu ya ishirini: Ni siku ya mazishi ambapo Mama Furaha anaisoma barua ya orodha. Padre James anajitahidi kumpinga mama Furaha asiisome orodha lakini hafanikiwi. Salim anapora barua na kuchana baadhi ya sehemu lakini hiyo haiharibu kitu kwani anaunga vipande na kusoma mbele ya wanakijiji wote. Ndani ya orodha hakuna jina la mtu yeyote lililotajwa bali mambo yatakayosaidia kuuepuka UKIMWI.




MTINDO



Mtindo aliotumia mwandishi ni wa dayalojia au majibizano. Mwandishi ameunda visa na masimulizi yake kupitia majibizano ya wahusika. Pia kwa kiasi kidogo ametumia mtindo wa monolojia, mfano uk. 27 padre James anasema:



“Bwana natazamiwa kuiendesha sala hiyo! Ni kitu ambacho hakikubaliki! Shetani yu kazini kjijini hapa! Furaha anavuna mbegu ya kifo aliyoipanda! Oh! Njia ya mtumishi wa bwana ni ngumu. Imejaa majaribu! Mtu lazima awe na nguvu na kuileta kazi ya bwana kwa watu hawa wa kawaida. Nimepewa kazi iliyo rahisi lakini ni ngumu sana! ni kazi ya upweke!!! Mwili ni mdhoofu! Oh Bwana utulinde.”



Hapa padre James aliongea mwenyewe akifikiri kuwaza na kujutia kazi anayofanya. Pia uk. Huohuo tunaona maneno ya Salim anaongea mwenyewe, pia uk.10, 23,37 na 40.



Pia mwandishi ametumia mtindo wa barua katika kazi yake lengo ikiwa ni kuweka mkazo katika mambo muhimu ya kuzingatia ili kuiepuka UKIMWI. Barua yenyewe ilisema hivi, uk.44“Kwa Kijiji changu kipendwa,



Nawasukuru kwa kufika kwenu na kuyasikiliza maneno yangu ya mwisho. Msiogope kwani nadhani maneno haya yanaweza kuwasaidia. Katika hii miezi ya mwisho nimelala kitandani nikifa, nikizidi kuugua. Nilipata muda mwingi wa kufikiri, kubadilika kukua kama mtu; hata ninapokuwa nakufa. Katika ukurasa unaofuata kuna Orodha ya vitu amabvyo vilisaidia kuyafupisha maisha yangu, orodha ambayo inaonesha kwenu nyote ukweli juu ya kifo changu. Mama, tafadhali wasomee watu wote orodha hii.

Uepukaji
Kondomu,
uaminifu ,
elimu,
welewa,
uwazi,
uadilifu,
uwajibikaji,
ukweli,
upendo,
msamaha.



Ukosefu wa mambo yote haya ndio ulioniua. Ufuatiliaji wa mambo yote haya unaweza kuwaokoa ninyi nyote. Chukueni orodha yangu na muinakili. Ipelekeni kwenye vijiji vingine, miji mingine na majiji mengine katika nchi yetu hii nzuri. Wanusuruni watu wetu ili waweze kuyafaidia maisha kikamilifu .Wanusuruni watoto wetu ili wasiwe yatima. Muinusuru Afrika…. Afrika yetu nzuri



Kwa kijiji changu kiishi maisha marefu na kiwe na furaha! Msihukukumu mapema mno. Kwa Mama, baba dada zangu, nawapenda. Jaribuni kuwa wenye furaha wakati mnaweza kufanya hivyo.Wenu awapendae Furaha.”




Matumizi ya nafsi



Mwandishi ametumia nafsi mbalimbali na hii ni mifano:

Nafsi ya kwanza umoja na wingi: Uk.28 Salim: “nilidhani sitakuona tena sijakuona muda mrefu”Uk.42 “oh huwezi kuamini jinsi tulivyojaribu”.
Nafsi ya pili: Salim : usifurahi kupita kiasiSalim: hufai kuhukumu unalala kama…..Mama Furaha: usiwe hivyo wewe u mtoto mzuri.
Nafsi ya tatu: Mama Furaha: kabla Furaha hajafa alitaka niahidi kumfanyia kitu fulani hapa kwenye mazishi ingawaje alikuwa na maumivu na mateso aliandika barua hii hapa na kunipa.




MATUMIZI YA LUGHA



Lugha aliyotumia mwandishi ni lugha fasaha na inayoleweka kwa wasomaji wake.




Matumizi ya tamathali za semi

Sitiari: Uk.2 “Waridi changa” “Ua kavu” –Mama anamfananisha Furaha na waridi au ua.Uk.4 “Nyie Mbu mlolaaniwa” –Baba Furaha anawaita wadogo zake Furaha;Uk.6 “Ua” –Furaha.Uk.25 “Slim”- UKIMWI. Wanakijiji wanaufananisha ugonjwa huu na jina hili kutokana na sifa yake ya kukondesha mwili.
Tashibiha: Uk.18 “yeye ni kama Punda wa kijiji”.Mwanakijiji wa 1 anamfananisha Furaha na Punda kutokana na tabia yake ya kuwa na wanume wengi. Malaya.Uk.13. “kisura ni kama jiji la New York…”Uk.43 “…vipande vinaanguka kama theluji”.
Mubaalagha: Uk.13 “kisura ni kama Jiji la New York ya Afrika Mashariki. Kule kuna majengoMajengo makubwa kiasi kwamba unaweza kuona mlima Kilimanjaro kwaJuu” pia anasema“Ndiyo mpenzi na Maduka… wana moja linaloitwaShoppers Plaza…! Pengine ndilo eneo kubwa lenye maduka makubwaKuliko yote katika Afrika”Uk.20 Furaha: nani aliyesema mambo hayo?Mama Furaha: Nusu ya kijiji kizima badala ya watu wengi. Mama Furahaanazidisha chumvi Kuonesha ukubwa wa hilo jambo.
Tafsida: Uk.7 maongezi kati ya wahusika;Mary: hiyo ni bia yake ya mwanzo.Furaha: ni chunguMary: ladha yake utaizoea tuBw. Juma: kama ulivyizoea wewe mayai yangu madogo!Bw. Ecko: Unaona! Inashangaza jinsi ambavyo mtu unaizoea haraka ladha hiyo!Bw. Juma:(kwa mary) kama ulivyofaanya wewe, mishikaki yangu midogo….Mazungumzo haya yamepunguza ukali wa maneno, maneno kama vile “Mishikaki” na “Mayai” ni sehemu za siri.




Mbinu nyingine za kisanaa

Mdokezo: Uk.8 “ndiyo padre….. ni …..”Uk.9 “Furaha…..fur….tuta…..”Uk.20 “ame…..tuseme…..”Uk.36 “misamaha padre mi…”Uk.44 “uepukaji….”
Nidaa: Uk.15 “Ooo!”Uk.34 “Oh!”Uk.41 “Eee”
Takriri: Uk.28 “Hapana hapana hapana nitauona!” “mpumbavu mpumbavu mimi”Uk.9 “hili ni jambo zito sana… sanasana…..sana hasa…”Uk 44 na 45 maneno haya yamerudiwa kuonesha msisitizo.Mwanakijiji wa 2: kondomMwanakijiji wa 3: elimuMwanakijiji wa 4: elimuMwanakijiji wa 1: uwaziKitunda: uadilifuPadre James: ukweliMary: upendoSalim: msamaha.
Tashtiti: Uk.20 mama Furaha: wewe na marafiki zako wa kiumeFuraha: marafiki gani wa kiume?Furaha anauliza swali ambalo majibu yake anayo ila tu anataka kuupindisha ukweli.Uk.38 baba: msalaba wako, padri. Uko shingoni mwako!Padre James: kweli?Baba: padre!Padre James: hakika?Padre James alijua wazi kuwa msalaba ulikuwa shingoni lakini kutokana na kutaka kuuficha ukweli alipokutwa katika pilika za kutafuta barua na kusingizia amedondosha msalaba. Alijifanya kuuliza kama vile hajui.
Onomatopea au tanakali sauti: Uk.33-34 “Myaau!” Uk.35 “Oooowww!”




Matumizi ya semi

Misemo:Uk.27 “Furaha anavuna mbegu ya kifo aliyopanda”




WAHUSIKA



FURAHA

Ni binti mdogo wa miaka kati ya 13-19
Ni Malaya
Anaathirika kwa ugonjwa wa UKIMWI
Alikuwa na bidii na mwenye kujituma
Ana tama
Ni mlevi
Ni mkweli na muwazi
Ni jasiri



BABA

Ni baba yake Furaha
Ni mkali
Ana upendo




MAMA FURAHA

Ni mama yake Furaha
Ni mkweli na muwazi
Ana upendo
Ni jasiri
Ni mchapakazi
Ni mpole
Ana msimamo
Anafaa kuigwa na jami




MARY

Ni binti mdogo
Ni Malaya
Si rafiki mwema
Anachangia kuharibu maisha ya Furaha
Ni mlevi
Anapenda anasa
Ana tama
Hafai kuigwa na jamii





BW. ECKO

Ni mwanaume mtu mzima
Ni Malaya
Si muaminifu katika ndoa yake
Ni mrubinifu kwa mabinti wadogo
Ni mlevi
Ni mfanyabiashara
Ni muathirika wa UKIMWI



JUMA

Ni mwanaume mtu mzima
Ni Malaya
Ni laghai kwa mabinti wadogo
Ni mlevi
Anapenda anasa
Ana tama
Ni rafiki wa Bw. Ecko




PADRI JAMES

Ni mtumishi wa Mungu katika kanisa katoliki
Si muadilifu
Anaogopa ukweli na uwazi
Ni dhaifu kwa wanawake
Anaweza kuwa ni muathirika wa UKIMWI



KITUNDA

Ni kijana wa mtaani
Anapenda anasa
Ana tama
Ni mlaghai kwa wasichana
Ni muhuni
Ni mlevi na mvuta bangi
Ana lugha ya kihuni



SALIM

Ni kijana wa kiume
Ni msomi
Ni mchumba wa Furaha
Anaweza kuwa ni muathirika wa UKIMWI
Si mkweli na muwazi
Si muadilifu
Wanakijiji 1,2 na 3
Ni wanakijiji katika kijiji cha Furaha
Hawana elimu juu ya UKIMWI
Ni wambea
Wana imani potofu



DADA MDOGO

Ni mdogo wake Furaha
Ana tabia njema
Ni mkweli lakini muoga
Hapendezwi na tabia ya dada yake




MANDHARI



Mandhari aliyotumia mwandishi ni ya vijiji vya Afrika Mashariki kwa ujumla wake. Mwandishi ametumia mandhari hii makusudi kwani imeendana na yale anayoyazungumza katika kitabu. Suala la ujinga na upotofu wa dhana kuhusu UKIMWI lipo zaidi vijijini. Wanakijiji hawaelewi juu ya UKIMWI. Mambo anayoyaibua mwandishi yanaendana na jamii ya watu wa vijiji hivyo mandhari ni sadifu.






Fani katika Tamthiliya ya Watoto wa Mama N’tiliye





MWANDISHI: EMMANUEL MBOGO



WACHAPISHAJI: HEKO PUBLISHERS



MWAKA: 2002




JINA LA KITABU



Jina la kitabu WATOTO WA MAMA NTILIE limesadifu yaliyomo ndani ya kitabu, kinaeleza kuhusu maisha ya watoto wa mama ntilie. Maisha ya dhiki, umaskini uliokithiri, maisha yasiyo ya faraja yaliyokosa malezi bora, chakula bora, elimu, huduma ya afya nk. Jina la kitabu linaakisi yaliyomo ndani ya kitabu na katika jamii yetu ya leo kwani akina mama wengi hawana kazi nzuri za kuwaingizia kipato kikubwa na bado wanategemewa katika malezi. Mwandishi ametumia jina hili ili kibua kero na matatizo yaliyoko katika jamii.




UTANGULIZI WA KITABU



Riwaya ya Watoto wa Mama N’tilie ni riwaya ambayo inasadifu maisha ya Mtanzania wa leo. Inaangazia suala la umaskini na hali ngumu ya maisha, wimbi la watoto wa mitaani, masuala ya uhalifu wizi na ujambazi, malezi nk. Mwandishi Mbogo amejitahidi sana. Pia katika fani ametumia muundo na mtindo wenye kuwavutia wasomaji pia kawaumba wahusika wake kwa usadifu wa hali ya juu huku mandhari yake ikiwa ni halisi inayosawiri maisha ya Tanzania.




MUUNDO



Muundo uliotawala katika riwaya hii ni muundo wa rukia au rejea. Mfano sura ya tatu mwandishi anatuelezea juu ya safari ya Mama ntilie kwenda matombo uk.34. Lakini anaacha kisa hicho ndani ya sura hiyohiyo anaanza kutuelezea juu ya kuzaliwa kwa watoto Kurwa na Doto na asili yao. Pia uk.80 mwandishi anatudokeza juu ya safari ya kwenda kwa Musa na hatuoneshi hatma ya safari yake bali anarukia kisa kingine na kuanza kutuelezea juu ya Zita kupandwa na kichaa uk.81. Vilevile uk.85-86 anatusimulia juu ya safari ya Mama Zita na Zenabu kuelekea hospitali kumwona Zita lakini hatuoneshi hatma ya safari yao bali anarukia kisa kingine na kuturudisha nyumbani kwa Mzee Lomolomo na jinsi anavyofakamia pombe alafu anaturudisha tena kutuambia juu ya kifo cha Zita hospitalini Muhimbili.



Mwandishi amegawa visa na matukio katika sura tano. Sura hizi zimejengwa katika muundo unaotegemeana ili kukamilisha kilele cha masimulizi.




MTINDO



Mtindo aliotumia mwandishi ni wa masimulizi ya mjazo au lugha ya nathari ameeleza visa mwenyewe na vingine wahusika wamevielezea. Pia ametumia mitindo kadha wa kadha. Mfano;Matumizi ya nafsi.

Nafsi ya tatu wingi na umoja: Uk.15 “Peter aliokota kipande cha muhogo” “alisafisha kipande cha muhogo”Uk.27 “walisaidiana wakaubeba” uk.26 “watu walisongamana walisukumana…..”.Kwa kiasi kikubwa matumizi ya nafsi ya tatu ndiyo yaliyotawala.
Nafsi ya kwanza umoja na wingi: Uk.58 “nitasema nitasema!”Uk.58 “njoo tuongee”Uk.56 “twende tule”.
Matumizi ya nafsi ya pili au dayalojia: Uk.89 pale Mama ntilie alipokumbuka majibizano yake na Zita.MAMA NTILIE: na hiyo nguo namna gani? Mbona chafu hivyo na leo ndio kwanza.Jumanne.PETER: mbwa Mama……ZITA: amenikwaruza kidogo na makucha yake.
Matumizi ya tanzu nyingine za kifasihi, mfano wimbo;Uk.78 “Jua ni moto,Tena ni mwangazaWa Dunia,Nadina yooNadina mama,Tumwombe Mungu Baba”Uk.10 wimbo alouimba mzee Lomolomo. “Kuleni nae,Hata bangi vuteni nae,Lakini ni kazi bure,Mwenzenu nimezaa naye,Pepepe kijani cha mbaazi,Kijaluba na msondoKiboko yao”.



Hivyo mwandishi ametumia mitindo hiyo ili kutomchosha msomaji mfano wimbo unamburudisha msomaji, majibizano yanavuta umakini zaidi na matumizi ya nafsi mbalimbali.




MATUMIZI YA LUGHA



Riwaya ya Watoto wa Mama Ntilie imetumia lugha rahisi, fasaha na inayoeleweka kwa wasomaji. Kuna matumizi ya lugha ya kiingereza mfano.Uk.36 “chloroquine”, “RosewinenaQueenElizabeth”,Uk.83 “faster faster mama” uk.1 “landrover”. Pia kuna matumizi ya lugha ya miitaaniuk.41 “kudeku…..”




Matumizi ya tamathali za semi

Tashibiha: uk.10 “mdomo wake ulio kaa kama bakuli la pombe”Uk.12 “mama ntilie alikaa kama kapigwa na radi”Uk.15 “miguu kama ya mamba”Uk.46 “aliinamisha shingo nayo ikapinda kama mforosadi” “kichwa kama stafeli”Uk.40. “kitovu chake kama jicho chongo”Uk.23 “Kurwa aliruka nyuma kama Chui”Uk.45 “akaruka kama Paa”
Tashihisi: Uk. 10 “mabega yenyewe tayari yalikuwa yamechongwa kwa pombe ya gongo.Yameangalia juu karibu yakutane na masikio”Uk.17 “aliziona nywele za kipilipili za Musa ngumu kama katani hazijaonja maji walasabuni”Uk.19 “ moshi wenye harufu ya kuudhi ulilelea hewani na kumlaki mtoto Peter.”Uk.35 “…… visogo vitatu vilikata kona na kupotea”Uk.46 “koo lilimsaliti”Uk.40 “miguuni raba zinazocheka kwa huzuni”Uk.46 “mlango ule wa kuungwa na gundi ulitika labeka”
Sitiari: Uk.10 “Nyama nyie”Uk.86 “…… wakatembea mwendo wa Farasi”
Ritifaa: Uk.38 “Mama? Mama yuko wapi, Baba yuko wapi? Mapenzi yao yako wapi?”Uk.92 “Zita! Zita! Zita! Zita umekwenda! Umenitoroka, Zita mwanangu”Uk.93 “Baba! Baba watoto? Mwenzangu! Ee! Amka, simama! Usiniachie tanzia hii peke Yangu”
Tafsida: Uk.91 “haja kubwa”




Matumizi ya mbinu nyingine za kisanaa

Onomatopea /tanakali sauti: Uk.5 “….. aliupinda mgongo kwa mbele akausikia unalia ka-ka-ka-ka, alitema mate tena Phuuuu”Uk.11 “alikohoa ukho! okho!”Uk.19 “…. Kwa kupiga chafya mbili au tatu Tcha! Tcha! Tcha!”Uk.50 “Bwee! Bwee! Bwee! Mbwa ….”Uk.50 “Hali … vicheko Woo! Woo! Weee! Weee! Heheheee! Leooo!”
Takriri: Uk.12 “twende! Twende! Nakuwacha nakauwacha!”Uk.58 “ Nivione! Nivione! Nivione vya kazi gani!”Uk.60 “ Nipishe! Nipishe! Nipishe!Uk.61 “kukurukakara, kukurukakara,kukurkakara”Uk.91 “ Baba! Baba! amka Baba”
Mjalizo: Uk. 40 “… akapata pesa, akala, akashiba”
Mdokezo: Uk.58 “usiseme hivyo! Unasikia ee! Usi……”Uk.71mara akaanza kuimba tena uleule wimbo wake wa “siwezi kuuwa mtu mama”Uk.73 “lakini…….”Uk.79 “ alikumbuka jaa laa jiji na ………”
Nidaa: Uk.44 “ Oh! Mungu wangu!”Uk.91 “ Mama wee!”Uk.90 “Hamadi! Mtume!”




Matumizi ya semi

Nahau: Uk.43 “…. Kupiga usingizi”
Methali: Uk.34 “ kamba hukatikia pembamba”Uk. 69 “fadhila za Punda”
Misemo: Uk.35 “ mtu wa maji” – mlevi.Uk.13 “kwake pombe ya mataputapu na gongo alivifanya dini”.




Matumizi ya taswira

Taswira mwonekano mfano: Uk.1 “ Mbwa huyu mweusi mwenye mkia mweupe, alionekana akitembea mwendo wa polepole. Ulimi wake mrefu ulionekana ukidondoka mate ya utelezi” hii inatufanya tupate picha halisi ya jinsi Mbwa huyo alivyo kupitia maneno ya msanii”.Uk.5 “….. hatua tatu mbele yake Sufuria, Vikombe na Sahani chafu zilizagaa pale nje zikimtazama. Akawaona nzi wakitembea na kurukaruka juu ya vyombo vichafu.Uk.10 “ mabega yenyewe tayari yalikuwa yamechonngoka kwa pombe ya gongo yameangalia juu karibu yakutane na masikio.”Uk.69 “Zenabu alibaki pale mlangoni kavaa gauni aina ya shifti, kitambaa cha Hariri”
Taswira hisi: Uk.91 “ Mzee Lomolomo alilala mdomo wazi Nzi wakubwa wa kijani kibichi wamejaa tele mdomoni mwake”.Hii inamfanya msomaji ajisikie kinyaa kutokana na hali hiyo ya Mzee Lomolomo anaposema nzi wa kijani kibichi, kwani hao ni nzi wanaokaa sana chooni na kwenye uchafu.




WAHUSIKA



Mama Ntilie

Ni mama mzazi wa Peter na Zita
Ni mke wa Mzee Lomolomo
Mlezi mzuri wa familia
Ni mvumilivu sana
Ana huruma
Ni mchapakazi na anayejituma
Ana hali ngumu kimaisha



Mzee Lomolomo

Ni mme wa mama ntilie
Baba wa Peter na Zita
Mlevi
Mvivu
Si mlezi bora hajali familia
Anakufa kwa sababu ya kunywa sana pombe



Peter

Mtoto wa mama ntilie
Anakosa elimu kwa sababu ya umaskini
Ana bidii na mchapakazi
Ana huruma
Anafungwa jela sababu ya kufanya biashara haramu ya madawa ya kulevya



Zita

Mtoto wa kike wa mama ntilie
Anakosa elimu sababu ya umaskini
Ni mchapakazi
Anagombana na Kurwa hakupenda aje kwao, roho mbaya
Anakufa kwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa



Doto

Ni mtoto yatima
Mtoto wa mtaani
Doto anauawa baada ya kujiingiza katika uhalifu wa wizi
Ni mgomvi na katili



Kurwa

Ni ndugu yake Doto
Anaishi mtaani
Ni yatima
Ana huruma
Ana nguvu na jasiri
Ni mchapakazi
Anaishia jela kwa sababu ya makosa ya Musa na Peter



Musa

Ni mtoto aliyekosa elimu baada ya kukosa sare na ada
Alikosa malezi mazuri ya wazazi
Mhalifu, anafanya biashara haramu za madawa ya kulevya
Ana tamaa ya pesa
Ni rafiki mbaya kwani alimshauri Peter kuuza madawa ya kulevya



Mwalimu Chikoya

Ni mwalimu wa akina Peter na Zita
Aliwafukuza Peter na Zita shule sababu ya kukosa ada
Si mwalimu mzuri




MANDHARI



Mandhari iliyotumika katika riwaya hii ni mandhari ya jiji la Dar es Salaam. Hii ni kutokana na kutajwa kwa maeneo ya jiji mfano, Manzese, Tabata, Kiwanda cha Urafiki, Kisutu, Muhimbili nk. Pia ametumia mandhari ya nyumbani mfano nyumbani kwa Mama Ntilie uk.5, mandhari ya hospitali ya Muhimbili uk.89, mandhari ya jaani-jaa la Tabata uk.20.



Kwa hiyo mwandishi ametumia mandhari inayosadifu aliyoyaeleza anaibua dhamira halisi zinazosawiri maisha ya Mtanzania wa leo kwa mandhari hiyo mfano suala la umaskini na wimbi la watoto wa mitaani.





Popular posts from this blog

UANDISHI WA INSHA NA MATANGAZO UANDISHI WA INSHA ZA KISANAA Insha za kisanaa ni insha zinazoelezea mambo ya kawaida katika jamii lakini kwa kutumia lugha ya kisanaa. Lugha ya kisanaa ni pamoja na matumizi ya tamathali za semi, misemo nahau, methali na taswira. Au, Insha ya kisanaa ni ile inayotumia lugha ya kisanaa yaani yenye tamathali za semi kama vile sitiari, tashbiha, taniaba na mubalagha. Aidha insha ya kisanaa hutumia mbinu nyingine za kisanaa kama tashititi, takriri, na tanakali sauti. Vilevile insha za kisanaa huwa na lugha zenye mvuto na misemo kama nahau, methali na tamathali za semi. Muundo wa Insha Kwa kawaida insha inakuwa na sehemu kuu nne: kichwa cha insha, utangulizi, kiini na hitimisho. a) Kichwa cha insha; Kichwa cha insha hudokeza kile utachokijadili katika insha yako, hubainisha wazo kuu la mada inayohusika. Kwa kawaida kichwa cha insha huandikwa kwa sentensi fupi. Mfano; maisha ya kijijini, mimba za utotoni. b) Utangulizi; Mambo yaliyopo katika utangul...
Uhakiki wa Fani katika Ushairi Fani katika Ushairi wa Wasakatonge Hakiki fani katika Ushairi wa Wasakatonge MWANDISHI: TAASISI YA KISWAHILI, ZANZIBAR WACHAPISHAJI: OXFORD UNIVERSITY PRESS MWAKA: 2001 JINA LA KITABU Jina la kitabu linasadifu yaliyomo katika kitabu. Kwa upande wa maudhui mambo yanayoelezwa mengi yanaigusa jamii ya sasa. Masuala ya maadili, siasa, uchumi, ukombozi wa kiutamaduni changamoto na suluhisho ya matatizo yanayoikumba jamii yanaendana na wakati wa sasa. Hivyo upya wa malenga wapya ni kweli. Kifani pia Malenga wapya wameweka muundo na mtindo wa kisasa. MUUNDO Tunapohakiki muundo katika ushairi tunaangalia idadi ya mistari katika ubeti. Ubeti huweza kuwa na mistari miwili, mitatu, minne na kuendelea. Aina za muundo zimepewa istilahi maalum kuutofautisha aina moja na nyingine mfano mashiri yenye mistari miwili katika ubeti ni Tathnia. Imetumika miundo tofautitofauti katika diwani hii. Mfano: Tathlitha: Haya ni mashairi ambayo ya...
MJENGO WA TUNGO Maana ya Tungo Tungo ni kipashio cha kisarufi kilichoundwa kwa kuunganisha pamoja vipashio vidogovidogo vilivyo chini yake. Au tungo ni neno au kikundi cha maneno ambacho hudokeza taarifa fulani ambayo huweza kuwa kamili au isiyo kamili. Kwa maana hii, tungo hujengwa na vipashio vidogovidogo kama vile mofimu kuunda neno, neno kuunda kirai, kirai kunda kishazi na kishazi kuunda sentensi. Kama tulivyokwisha kuona hapo juu tungo huanzia neno; rejea aina za tungo. AINA ZA TUNGO Tungo neno: Tungo neno ni tungo ambayo huundwa na vipashio vidogo zaidi ya neno ambayo ni mofimu au fonimu. Mfano; anacheza, kakimbia. Tungo Kirai: ni kipashio cha kimuundo chenye neno moja au zaidi lakini ambacho hakina muundo wa kiima kiarifu. Mfano; mtoto mzuri, kiyama chake, bondeni Tungo kishazi: Kishazi ni tungo yenye kitenzi ambacho chaweza kujitosheleza na kukamilisha ujumbe uliokusudiwa na mzungumzaji au kuwa na kitenzi kisichoweza kujitegemea chenyewe. KI...
NGELI ZA MANENO Upatanishi wa Kisarufi katika Sentensi Ngeli ni vikundi vya majina ya Kiswahili. Ngeli za nomino ni utaratibu unaotumika kuweka nomino katika matabaka au makundi yanayofanana. Mfano: 1. Maji yakimwagika hayazoleki 2. Mayai yaliyooza yananuka sana 3. Yai lililooza linanuka sana 4. Maji liliomwagika halizoleki Katika mifano hii tunaona kwamba sentensi a, b na c ziko sahihi wakati sentensi d sio sahihi, hii ni kwa sababu imekiuka upatanisho wa kisarufi. Kwa maana hiyo sentensi ‘a’ ipo katika ngeli ya YA-YA na senthensi b na c zipo katika ngeli ya LI-YA. Sentesi d sio sahihi kwa sababu nomino maji haina wingi, kwa hiyo haiwezi kuingia katika ngeli ya LI-YA. Kwa msingi huu ngeli za nomino huzingatia sana upatanisho wa kisarufi. Jedwali lifuatalo huonesha ngeli za nomino kwa misingi ya upatanisho wa kisarufi. Baadhi ya matumizi ya ngeli ni pamoja na haya yafuatayo: 1. Hutumika kupanga majina ya lugha k...
MAENDELEO YA KISWAHILI ASILI YA KISWAHILI Neno asili ni jinsi kitu au jambo lilivyotokea au lilivyoanza. Kutokana na fasili hii tunaona kwamba jambo au kitu kinaweza kutokea kibahati kama ilivyo katika lugha au linaweza kuanzishwa. Hivyo basi asili ya lugha ya Kiswahili bado ni mjadala mrefu ambapo wataalamu mbalimbali wanahitilafiana juu ya asili au chimbuko la lugha ya kiswahili. Wapo wanaokinasibisha kiswahili na kiarabu kwa kutumia kigezo cha msamiati na dini ya kiislamu. Wengine wanashikilia msimamo kuwa kiswahili ni kibantu kwa kutumia hoja za kiisimu na kihistoria. Wapo wanaokinasibisha kiswahili na uchotara baadhi yao wanaoshikilia msimamo huu ni Freeman Grenville na Homo Sasson Kuna nadharia mbalimbali zinazojaribu kuelezea asili ya Kiswahili, miongoni mwa hizo ni pamoja na hizi zifuatazo: Kiswahili ni Kiarabu Hapa Kiswahili kimefasiliwa kuwa asili yake ni kiarabu, wanaoshikilia mtazamo huu wanahoji kwamba katika lugha ya Kiswahili kuna maneno mengi ya Ki...