Skip to main content


UANDISHI WA INSHA NA MATANGAZO


UANDISHI WA INSHA ZA KISANAA


Insha za kisanaa ni insha zinazoelezea mambo ya kawaida katika jamii lakini kwa kutumia lugha ya kisanaa. Lugha ya kisanaa ni pamoja na matumizi ya tamathali za semi, misemo nahau, methali na taswira. Au, Insha ya kisanaa ni ile inayotumia lugha ya kisanaa yaani yenye tamathali za semi kama vile sitiari, tashbiha, taniaba na mubalagha. Aidha insha ya kisanaa hutumia mbinu nyingine za kisanaa kama tashititi, takriri, na tanakali sauti. Vilevile insha za kisanaa huwa na lugha zenye mvuto na misemo kama nahau, methali na tamathali za semi.


Muundo wa Insha
Kwa kawaida insha inakuwa na sehemu kuu nne: kichwa cha insha, utangulizi, kiini na hitimisho.
a) Kichwa cha insha; Kichwa cha insha hudokeza kile utachokijadili katika insha yako, hubainisha wazo kuu la mada inayohusika. Kwa kawaida kichwa cha insha huandikwa kwa sentensi fupi. Mfano; maisha ya kijijini, mimba za utotoni.
b) Utangulizi; Mambo yaliyopo katika utangulizi ni pamoja na kutoa fasili ya maneno muhimu na kuelezea kwa muhtasari mambo ambayo utakwenda kuyajadili katika insha yako. Utangulizi unakuwa katika aya moja fupi.
c) Kiini cha insha; Katika kiini ndipo kuna maelezo ya kina juu ya kile unachokijadili katika insha yako, maelezo haya yanakuwa katika aya kadhaa kulingana na idadi ya hoja ulizonazo katika mjadala wako.
d) Hitimisho; Hapa ndipo kuna muhtasari wa kile kilichojadiliwa katika kiini cha insha au inaweza kuwa ni msimamo juu ya kile kilichojadiliwa katika insha.

UANDISHI WA MATANGAZO



Tangazo ni taarifa za wazi zinazotoa ujumbe fulani kwa walengwa wanaohusika na ujumbe huo. Ujumbe unaweza kuwa na lengo la kushawishi, kuarifu, kuelekeza, na kadhalika.


Vipengele vya Kuzingatiwa katika Uandishi wa Mtangazo


Malengo ya Matangazo
1. Kutoa taarifa; Lengo mojawapo la matangazo ni kutoa taarifa, mfano wa matangazo yanayotoa taarifa ni mialiko, tangazo la kifo, alama za barabarani, matangazo ya kazi.
2. Kuonya; Matangazo pia yana lengo la kuonya, kwa mfano matangazo kama vile ya kutovuta sigara, UKIMWI na kadhalika.
3. Kushawishi; Matangazo pia yana lengo la kushawishi, matangazo yenye lengo hili mara nyingi ni matangazo ya biashara ambayo kwa kweli lengo lake ni kushawishi wateja ili wanunue bidhaa zao, mtangazo ya mialiko hasahasa ya tukio fulani, labda msanii anazindua albamu fulani na kadhalika.





Jinsi ya Kuandika Matangazo


Ili tangazo liweze kufanikisha kufikia lengo lililokusudiwa kuna mambo kadhaa ya kufanya; mambo hayo ni kama yafuatayo:
1. Kichwa cha habari; Mara nyingi matangazo yanakuwa na kichwa cha habari, hii inasaidia kujua kwa haraka kuwa tangazo linahusika na kitu gani.
2. Kuonesha aina ya bidhaa/huduma; Hiki ndicho kiini cha tangazo, hapa tangazo linaonesha ujumbe uliokusudiwa kufikishwa kwa wahusika, sasa ujumbe huu waweza kuwa ni bidhaa inayotangazwa au huduma inayotolewa au kazi inayotangazwa au mwaliko unahusu nini.
3. Anwani; Hapa tangazo linaonesha mahali ambapo watoa tangazo walipo, yaani ofisi zao zilipo ambapo wahusika wa tangazo wanaweza kwenda na kuwakuta. Kama ni tangazo la mwaliko basi ni lazima lionesha shughuli yenyewe itafanyika wapi.
4. Njia za mawasiliano; Kama ni tangazo la biashara au la kazi au la mwaliko ni muhimu kutoa mawasiliano. Mawasiliano hayo yanaweza kuwa ni namba ya simu, fax, wavuti (kwa taarifa zaidi), barua pepe.






Mbinu za Uandishi wa Matangazo


Ili tangazo liweze kuvuta umakini wa watu ni lazima liwe na mwonekanao fulani. Zifuatazo ni mbinu za uandishi wa matangazo.
1. Matumizi ya picha; Matangazo mengi ya biashara huwa yanaambatana na picha, picha hizi hujaribu kumshawishi mteja aamini kuwa ile bidhaa ni bora na hivyo ni muhimu kuwa nayo au kuinunua.
2. Maneno machache; Matangazo hutumia maneno machache kwa lengo la kutomchosha mlengwa lakini wakati huohuo maneno hayo yana nguvu ya kumshawishi mlengwa.
3. Lugha ya kisanii; Maneno ya kisanii katika matangazo huwa ni mepesi kukumbukwa na huwa yanaeleweka kirahisi. Kwa mfano, matumizi ya vivumishi, litakuwa ni bonge la shoo, njoo ujinunulie pamba za ukweli, n.k. Matumizi ya mubalagha, kwa mfano; mtandao unaoongoza Tanzania, mganga bingwa afrika mashariki na kati n.k
4. Matumizi ya watu maarufu; Matangazo mengi hususani ya biashara hupenda kutumia watu maarufu ili kuwashawishi walengwa. Kwa mfano kama ni tangazo juu ya bidhaa fulani, huweza kumwonesha pengine msanii maarufu, miss Tanzania, au mchezajia mpira maarufu. Sasa mlengwa anapoona kwamba hata mtu maarufu anatumia hiyo bidhaa, anashawishika na yeye kuitumia.

Popular posts from this blog

Uhakiki wa Fani katika Ushairi Fani katika Ushairi wa Wasakatonge Hakiki fani katika Ushairi wa Wasakatonge MWANDISHI: TAASISI YA KISWAHILI, ZANZIBAR WACHAPISHAJI: OXFORD UNIVERSITY PRESS MWAKA: 2001 JINA LA KITABU Jina la kitabu linasadifu yaliyomo katika kitabu. Kwa upande wa maudhui mambo yanayoelezwa mengi yanaigusa jamii ya sasa. Masuala ya maadili, siasa, uchumi, ukombozi wa kiutamaduni changamoto na suluhisho ya matatizo yanayoikumba jamii yanaendana na wakati wa sasa. Hivyo upya wa malenga wapya ni kweli. Kifani pia Malenga wapya wameweka muundo na mtindo wa kisasa. MUUNDO Tunapohakiki muundo katika ushairi tunaangalia idadi ya mistari katika ubeti. Ubeti huweza kuwa na mistari miwili, mitatu, minne na kuendelea. Aina za muundo zimepewa istilahi maalum kuutofautisha aina moja na nyingine mfano mashiri yenye mistari miwili katika ubeti ni Tathnia. Imetumika miundo tofautitofauti katika diwani hii. Mfano: Tathlitha: Haya ni mashairi ambayo ya...
MJENGO WA TUNGO Maana ya Tungo Tungo ni kipashio cha kisarufi kilichoundwa kwa kuunganisha pamoja vipashio vidogovidogo vilivyo chini yake. Au tungo ni neno au kikundi cha maneno ambacho hudokeza taarifa fulani ambayo huweza kuwa kamili au isiyo kamili. Kwa maana hii, tungo hujengwa na vipashio vidogovidogo kama vile mofimu kuunda neno, neno kuunda kirai, kirai kunda kishazi na kishazi kuunda sentensi. Kama tulivyokwisha kuona hapo juu tungo huanzia neno; rejea aina za tungo. AINA ZA TUNGO Tungo neno: Tungo neno ni tungo ambayo huundwa na vipashio vidogo zaidi ya neno ambayo ni mofimu au fonimu. Mfano; anacheza, kakimbia. Tungo Kirai: ni kipashio cha kimuundo chenye neno moja au zaidi lakini ambacho hakina muundo wa kiima kiarifu. Mfano; mtoto mzuri, kiyama chake, bondeni Tungo kishazi: Kishazi ni tungo yenye kitenzi ambacho chaweza kujitosheleza na kukamilisha ujumbe uliokusudiwa na mzungumzaji au kuwa na kitenzi kisichoweza kujitegemea chenyewe. KI...
NGELI ZA MANENO Upatanishi wa Kisarufi katika Sentensi Ngeli ni vikundi vya majina ya Kiswahili. Ngeli za nomino ni utaratibu unaotumika kuweka nomino katika matabaka au makundi yanayofanana. Mfano: 1. Maji yakimwagika hayazoleki 2. Mayai yaliyooza yananuka sana 3. Yai lililooza linanuka sana 4. Maji liliomwagika halizoleki Katika mifano hii tunaona kwamba sentensi a, b na c ziko sahihi wakati sentensi d sio sahihi, hii ni kwa sababu imekiuka upatanisho wa kisarufi. Kwa maana hiyo sentensi ‘a’ ipo katika ngeli ya YA-YA na senthensi b na c zipo katika ngeli ya LI-YA. Sentesi d sio sahihi kwa sababu nomino maji haina wingi, kwa hiyo haiwezi kuingia katika ngeli ya LI-YA. Kwa msingi huu ngeli za nomino huzingatia sana upatanisho wa kisarufi. Jedwali lifuatalo huonesha ngeli za nomino kwa misingi ya upatanisho wa kisarufi. Baadhi ya matumizi ya ngeli ni pamoja na haya yafuatayo: 1. Hutumika kupanga majina ya lugha k...
MAENDELEO YA KISWAHILI ASILI YA KISWAHILI Neno asili ni jinsi kitu au jambo lilivyotokea au lilivyoanza. Kutokana na fasili hii tunaona kwamba jambo au kitu kinaweza kutokea kibahati kama ilivyo katika lugha au linaweza kuanzishwa. Hivyo basi asili ya lugha ya Kiswahili bado ni mjadala mrefu ambapo wataalamu mbalimbali wanahitilafiana juu ya asili au chimbuko la lugha ya kiswahili. Wapo wanaokinasibisha kiswahili na kiarabu kwa kutumia kigezo cha msamiati na dini ya kiislamu. Wengine wanashikilia msimamo kuwa kiswahili ni kibantu kwa kutumia hoja za kiisimu na kihistoria. Wapo wanaokinasibisha kiswahili na uchotara baadhi yao wanaoshikilia msimamo huu ni Freeman Grenville na Homo Sasson Kuna nadharia mbalimbali zinazojaribu kuelezea asili ya Kiswahili, miongoni mwa hizo ni pamoja na hizi zifuatazo: Kiswahili ni Kiarabu Hapa Kiswahili kimefasiliwa kuwa asili yake ni kiarabu, wanaoshikilia mtazamo huu wanahoji kwamba katika lugha ya Kiswahili kuna maneno mengi ya Ki...
UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI Fasihi andishi ni tawi la fasihi linalotumia sanaa ya maneno kufikisha ujumbe kwa hadhira kwa njia ya maandishi. Zipo aina nyingi za fasihi andishi, miongoni mwa hizo ni pamoja na hadithi fupi, riwaya, tamthiliya na mashairi. Maana ya Uhakiki Dhana ya Uhakiki Fafanua dhana ya uhakiki Uhakiki ni kitendo cha kutathimini, kueleza, kuainisha na kutoa maoni juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalum. Hii ina maana kwamba uhakiki wa kazi za fasihi hautoki katika ombwe, kuna kanuni na taratibu mbalimbali zinazoongoza kufanya uhakiki, na hii ndio sababu kuna nadharia kadha wa kadha za uhakiki wa kazi za kifaishi. AU kwa lugha rahisi tunaweza kusema, uhakiki ni uchambuzi wa kina wa kazi za fasihi kama vile riwaya, tamthiliya na mashairi kwa lengo la kufafanua vipengele vya fani na maudhui. Misingi ya Uhakiki Elezea misingi ya uhakiki Kwa ujumla mhakiki wa kazi za fasihi anapofanya uhakiki wa kazi za kifasihi,...